Michezo

Peres Jepchirchir abadilisha muda anaotupia jicho

October 24th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI mpya wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya wanawake duniani, Peres Jepchirchir amebadilisha lengo lake katika mbio zake za kufunga mwaka 2020 za Valencia Marathon zitakazofanyika Desemba 6.

Aliponyakua taji la dunia mjini Gdynia nchini Poland wiki moja iliyopita (Oktoba 17), Jepchirchir alisema anatupia jicho kutimka mbio za kilomita 42 mjini Valencia nchini Uhispania kwa kati ya saa 2:18 na 2:19. Sasa kutimka kwa kasi ya juu zaidi. Amepandisha lengo la muda anaotafuta kuwa kati ya saa 2:17 na 2:18.

“Msimu wangu bado haujakamilika. Nitashiriki mbio za Valencia Marathon mwezi Desemba kwa hivyo ninajiandaa vilivyo kwa mbio hizo. Nadhani kuibuka bingwa wa Nusu-Marathon Duniani katika muda ambao ni rekodi ya dunia (saa 1:05:16) kumenipa motisha. Ningependa kukamilisha mbio za Valencia kwa saa 2:17 ama 2:18,” Jepchirchir amenukuliwa na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOC-K) akisema Oktoba 23.

Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atakuwa Mkenya wa tatu katika historia ya miaka 39 ya Valencia Marathon akitwaa taji baada ya Gladys Chebet (2010) na Valary Aiyabei (2016). Bingwa wa mwaka 2019 Roza Dereje anashikilia muda bora wa wanawake wa Valencia Marathon baada ya kubeba taji kwa saa 2:18:30 wakati Kinde Atanaw pia kutoka Ethiopia aliibuka mfalme kwa rekodi ya Valencia Marathon ya wanaume ya saa 2:03:51.

Rekodi za dunia za wanawake na wanaume za mbio za kilomita 42 zinashikiliwa na Wakenya Mary Keitany (2:17:01) na Eliud Kipchoge (2:01:39), mtawalia.