Michezo

Peres Jepchirchir aweka rekodi mpya Marathon ya wanawake

April 21st, 2024 2 min read

Na AYUMBA AYODI

WAKENYA Peres Jepchirchir na Alexander Mutiso Munyao walipata ushindi wao wa kwanza katika mbio za London Marathon huku bingwa wa Olimpiki wa wanawake akivunja rekodi ya dunia ya wanawake pekee.

Ilikuwa mara ya kwanza Wakenya kushinda mataji yote tangu 2019, wakati bingwa wa Marathon katika Olimpiki Eliud Kipchoge na Brigid Kosgei waliposhinda.

Jepchirchir alishinda kwa urahisi kwa saa mbili, dakika 16 na sekunde 16 kuvunja rekodi ya dunia ya wanawake pekee kwa sekunde 45, akifuta muda uliopita wa 2:17:01 uliowekwa na Mkenya Mary Keitany mwaka 2017.

Jepchirchir 30, bingwa mara tatu wa mbio za dunia za 21KM, alimshinda mwanariadha wa rekodi ya dunia ya marathon Tigst Assefa kutoka Ethiopia katika kilomita ya mwisho.

Assefa, bingwa wa Berlin Marathon wa 2022 na 2023, alimaliza wa pili kwa saa 2:16:23 huku bingwa wa London Marathon wa 2021 Joyciline Jepkosgei, akimaliza wa tatu kwa saa 2:16:24.

Ushindi wa Jepchirchir, wa tatu katika Marathon Majors ya Dunia baada ya New York City Marathon ya 2021 na Boston Marathon ya 2022, umeimarisha nafasi yake katika timu ya marathon kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris.

Munyao, ambaye alikuwa akiingia mara yake ya kwanza katika London na Marathon Majors ya Dunia, alikuwa mshindi wa kushangaza katika wanaume kwa saa 2:04:01.

Munyao mwenye umri wa miaka 27, ambaye alikuwa akishiriki mara yake ya nne ya marathon, alikabiliana uso kwa uso na mwanariadha mkongwe kutoka Ethiopia Kenenisa Bekele katika kilomita 12 za mwisho kabla ya kumshinda kwa mbali katika kilomita saba za mwisho.

Bekele alimaliza wa pili kwa 2:04:15 akifuatiwa na Waingereza Emile Cairess na Mahamed Mahamed kwa muda bora wa 2:06:46 na 2:07:05 mtawalia.

Ilikuwa mara ya nne ya Munyao kushiriki katika mbio, baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika mbio za Tokyo mwaka 2020 lakini akashindwa kumaliza mbio.

Munyao alishindana tena katika Valencia Marathon ya 2022 ambapo alimaliza wa tatu kwa muda bora wa 2:03:29 ambapo  alishirikiana na emu Kelvin Kiptum, ambaye alishinda kwa muda wa 2:01:53.

Hii ilimfanya Kiptum kuwa mwanariadha wa tatu kasi zaidi wakati huo huku muda wa Munyao ukimfanya kuwa mtu wa 20 kasi zaidi katika historia ya mbio hizo.

Mnamo Mei 7, 2023, Munyao alishinda Prague Marathon kwa saa 2:05:09 kabla ya kurudi Valencia mwezi Desemba mwaka huo na kumaliza wa pili kwa muda wa 13 kasi zaidi wa 2:03:11, mbio zilizoshindwa na Mhabeshi Sisay Lemma wa nne kasi zaidi na muda wa 2:01:48.

Bekele alimaliza wa nne katika mbio hizo kwa muda wa 2:04:19.

Wakenya sasa wameshinda katika matoleo matatu ya mwisho ya London Marathon huku Kiptum akiibuka mshindi mwaka 2023 kwa muda wa rekodi nzuri zaidi ya muda wa 2:01:25, akifuta muda wa awali wa 2:02:37 uliowekwa na Eliud Kipchoge mwaka 2019.