Michezo

Peres Jepchirchir kuongoza Wakenya kumenyana na Waethiopia katika Valencia Half Marathon

October 5th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za Nusu Marathon, Peres Jepchirchir, ni miongoni mwa Wakenya watakaonogesha mbio za kilomita 21 za Valencia Half Marathon mnamo Disemba 6, 2020.

Jepchirchir atatoana jasho na Wakenya Joan Chelimo, Fancy Chemutai na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya nusu marathon duniani, Joyciline Jepkosgei.

Mbio hizo zimevutia pia mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 10,000 duniani, Letesenbet Gidey wa Ethiopia ambaye atakuwa akishiriki mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza.

Sheila Chepkirui, ambaye ni mwanamke wa pili mwenye kasi ya juu zaidi katika mbio za kilomita 10 (dakika 29:46) pia atashiriki mbio hizo zitakazonogeshwa na mshindi wa medali ya fedha katika mbio za mita 5,000 duniani mnamo 2015, Senbere Teferi. Teferi ndiye alitawala mbio za Valencia Half Marathon mnamo 2019 kwa muda wa saa 1:05:32.

Katika miaka ya hivi karibuni, jiji la Valencia nchini Uhispania limekuwa jukwaa la wanariadha kuvunja baadhi ya rekodi kwenye mbio za masafa marefu.

Rekodi mbili za dunia katika mbio za kilomita 10 kwa upande wa wanaume na mbili nyinginezo katika mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanawake zilivunjwa jijini Valencia.

Rekodi za dakika 58:18 saa 1:04:51 ambazo ziliwahi kuandikishwa katika mbio za Valencia Half Marathon sasa zitakuwa katika hatari ya kuvunjwa mnamo Disemba 6, 2020. Rekodi za dunia katika nusu marathon ni dakika 58:01 na saa 1:04:31 kwa upande wa wanaume na wanwake mtawalia.

Mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani Rhonex Kipruto atakuwa miongoni mwa wanariadha watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Nusu Marathon ya Valencia.

Mtimkaji huyo aliyeweka rekodi ya dakika 26:24 kwenye mbio za kilomita 10 jijini Valencia mapema mwaka wa 2020, atarejea Uhispania kushiriki mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza. Mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za nyika duniani, Jacob Kiplimo wa Uganda ni kati ya wanariadha wanaotazamiwa kumtoa Kipruto kijasho.

Wanariadha wengine 10 watakaonogesha kivumbi hicho cha Valencia Half Marathon ni bingwa wa Ras Al Khaimah Half Marathon mnamo 2015 Stephen Kiprop, Bedan Karoki aliyeridhika na nishani ya fedha katika mbio za kilomita 21 duniani mnamo 2016 na Bernard Ngeno aliyeambulia nafasi ya pili kwenye Valencia Half Marathon mnamo 2019.

Wengine ni mshikilizi wa rekodi ya bara Ulaya katika mbio za kilomita 21, Julien Wanders wa Uswisi na bingwa wa Afrika katika mbio za nyika, Alfred Barkach.

Muda bora na wa kasi zaidi huenda ukashuhudiwa kwenye mbio za kilomita 42 ambazo zimevutia wanariadha wa haiba kubwa akiwemo bingwa wa Tokyo Marathon mnamo 2019, Ruti Aga (2:18:34) atakayetoana jasho na Mwethiopia mwenzake Birhane Dibaba (2:18:35).

Mare Dibaba, aliyeibuka bingwa wa dunia katika marathon mnamo 2015 pia atanogesha kivumbi cha Valencia Marathon kwa pamoja na Waethiopia Zeineba Yimer na Tigist Girma wanaojivunia muda wa chini ya saa 2:20. Jordan Hasay wa Amerika pia atakuwa sehemu ya washiriki wa mbio hizo kwa upande wa wanawake.

Kwa upande wa wanaume, Kinde Atanaw, aliyeweka rekodi ya saa 2:03:51 mnamo 2019, atalenga kuhifadhi ufalme wake japo atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Mwethiopia mwenzake, Birhanu Legese ambaye anajivunia muda wa tatu wa kasi zaidi katika mbio za mita 42 (2:02:48).

Wanariadha wengine ambao wamethibitisha kushiriki mbio hizo za Valencia Marathon ni bingwa wa zamani wa dunia Lelisa Desisa, bingwa wa Boston na Chicago Marathon Lawrence Cherono, mshikilizi wa rekodi ya bara Ulaya Kaan Kigen Ozbilen na mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 21 nchini Ethiopia, Jemal Yimer. Itakuwa mara ya kwanza kwa Yimer kunogesha mbio za kilomita 42.