Habari

Pesa kutiririka katika kaunti sasa baada ya Uhuru kutia saini mswada wa CARA

October 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta, Alhamisi, Oktoba 8, 2020, ametia saini Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARA) ambao unatoa nafasi kwa usambazaji wa fedha kwa kaunti zote 47.

Mswada huo ulipitishwa na Bunge la Kitaifa mnamo Jumanne baada ya kupitishwa katika bunge la seneti majuma mawili yaliyopita.

Rais Kenyatta ameutia saini mswada huo mwendo wa asubuhi katika Ikulu ya Nairobi, katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka. Wengine waliokuwepo ni kiongozi wa wengi katika Seneti Samuel Poghisio na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Amos Kimunya.

Sheria hiyo inatoa mwongozo wa namna jumla ya Sh369.87 bilioni zilizotengewa kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.

Fedha hizo zinajumuisha Sh316.5 bilioni ambao utagawanywa kwa njia sawa baina ya kaunti na Sh13.73 bilioni kama ruzuku kutoka Serikali ya Kitaifa. Fedha hizo pia zinajumuisha Sh9.43 bilioni za kufadhiliwa utunzaji wa barabara katika kaunti na Sh30.2 bilioni ambazo ni mikopo na ruzuku kutoka nje.

Ruzuku kutoka serikali ya kitaifa zitatumiwa katika ulipaji wa ada ya kila mwezi ya ukodishaji wa vifaa vya kisasa vya kimatibabu (MES) na ukarabati wa vyuo anuai katika kaunti zote 47.

Mswada huo ulipitishwa na Maseneta mnamo Septemba 29 baada ya mwao kuvutana kwa miezi mitatu kuhusu mfumo bora wa kugawanya fedha hizo baina ya kaunti. Hii ni baada ya wao kukataa mfumo uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ambao ulifanyiwa mabadiliko na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha.

Mfumo huo ulikataliwa baada ya kubainika kuwa ungechangia kaunti 18 kupoteza kima cha Sh17 bilioni ikilinganishwa na zile ambazo zilipokea katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020. Wakati huo huo, kaunti 29 zenye idadi za juu za watu zingeongezewa mabilioni ya fedha chini ya mfumo huo, uliokipa kigezo cha idadi ya watu uzito mkubwa.

Tangu Julai 1, 2020, mwaka huu wa kifedha ulipoanza, serikali za kaunti zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha hali iliyosababisha Baraza la Magavana (CoG) kuamuru kusitishwa kwa shughuli mnamo Septemba 17. Hii ni baada ya kaunti kadha kukosa kuwalipa wafanyakazi wao mishahara kwa kipindi cha takriban miezi mitatu.

Tayari Waziri wa Fedha Ukur Yattani ametangaza kuwa Sh60 bilioni ziko tayari kusambazwa kwa kaunti.

Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o amesema kuwa kaunti tatu pekee ndizo hazijawasilisha bajeti zao na hivyo hazitapokea fedha kutoka Hazina ya Kitaifa.

“Kaunti 44 zimewasilisha bajeti zao katika afisi yangu na zitaanza kupokea fedha zao kuanzia Ijumaa, Oktoba 9, 2020. Kaunti tatu zilizosalia zitatumiwa fedha pindi zitakapowasilisha bajeti zao,” Dkt Nyakang’o akaambia Taifa Leo.