Pesa za wizi hazina maana, akiri pasta

Pesa za wizi hazina maana, akiri pasta

Na MWANGI MUIRURI

PASTA Cyrus Njora wa Kanisa la Maximum Miracle Centre amefungua roho yake na kukiri jinsi alivyokuwa jambazi sugu aliyeshiriki wizi wa zaidi ya magari 100 yaliyompa zaidi ya Sh27 milioni kutoka soko la taifa mojawapo la ukanda wa Afrika Mashariki.

Anakiri kuwa alianza kwa kujifanya mteja wa ukodishaji magari ambayo aliishia kuyauza katika taifa hilo jirani na kisha akawa katika genge la kujihami ambalo liliiba mengine zaidi kimabavu.

Pasta Njora anasema kuwa katika kipindi cha miaka miwili aliyokuwa katika mtandao huo wa ujambazi, wenzake sita waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi huku yeye akiponea siku ya sadfa.

Kinachomkera zaidi ni kuwa licha ya wizi huo uliomvunia mamilioni, alipokamatwa mwaka wa 2008 na akahukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani, hakuwa hata na ndururu.

“Leo hii nina ushuhuda kwamba pesa za wizi hazitawahi kukufaa. Hatari ya ujambazi hata sio kukamatwa au kuuawa ana na raia au polisi, bali uchungu ni kuishia kuteseka ukiwa huna hata ndururu,” asema.

Pasta Njora anasema kuwa katika kilele chake cha ujambazi, angetia mkobani takriban Sh100,000 asubuhi na zote kabla ya jua kutua ziwe zimetumika katika raha na anasa ya ulevi, nyama choma na mahaba.

“Ujambazi hukupa raha tupu isiyo na kifani. Kuna ile kasumba kwamba ukiwa na pesa hutakuwa na bidii ya kutafuta tena na tena. Ujinga ndani ya bongo la jambazi ni sawa na ushetani. Utapata majambazi katika mikutano ya maandalizi ya mikakati yao wakijigamba jinsi walivyochoma maelfu kwa siku moja tu lakini siku ya kukamatwa na kuhukumiwa, hata adaiwe faini ya Sh10,000 pekee, utapata hana,” asema.

Pasta Njora anasema kuwa alipozaliwa katika kijiji cha Ichamara katika Kaunti ya Nyeri mwaka wa 1985, wazazi wake walikuwa na dua njema tu kwake na alipojiunga na Shule ya Msingi ya Kihate na kisha akajiunga na ile ya Upili ya Tambaya ambapo aliokoka mwaka wa 2000 akiwa Kidato cha Pili, ndoto yake ilikuwa aishie kuwa daktari wa upasuaji.

“Lakini nilipata alama ya C katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka wa 2002 na kukosa mwaliko wa kujiunga na chuo kikuu na ikizingatiwa ukata katika familia yetu, ikawa tamati ya masomo yangu. Lakini walinifadhili nikasomea udereva,” asema.

Ni katika hali hiyo ambapo mnamo Februari 10, 2003, aliondoka nyumbani akiandamana na rafiki yake aliyekuwa amemtangulia jijini Nairobi na akapata kazi ya kuuza kanda za muziki katika mtaa wa River Road.

“Ni katika kukumbatia ushauri wazazi wangu walionipa nikiondoka nyumbani wakinihimiza nijichunge na athari za anasa na kutojielewa kimaisha katika jiji kuu ambapo nilichapa kazi kwa bidii na kwa siku ningejipata nikiwa na faida ya Sh1,000,” asema.

Mwaka wa 2005, Pasta Njora alikuwa ameweka akiba iliyomwezesha kufungua duka lake la kanda za muziki jijini Nairobi.

Kijana aliyekuwa ameonyesha nia ya kufaulu katika maisha yake aligeuka ghafla mwaka wa 2006.

“Nikiwa katika duka langu, kuna wanafunzi wawili; mmoja wa kike na mwingine wa kiume waliokuja na wakaniachia mikoba yao ya shule. Tulikuwa tunafahamiana. Mimi hata sikuangalia ni nini kilikuwa ndani ya mikoba hiyo. Lakini muda baadaye, yule kijana alirejea na akachukua mkoba mmoja. Saa chache baadaye, yule msichana alikuja na alipodai mkoba wake, ukawa hauko. Kumbe wake ulikuwa na kipakatalishi na ndio uliochukuliwa na yule kijana! Mambo yakageuka kuwa balaa tupu,” asema Pasta Njora.

Maisha ya rumande

Mwanafunzi huyo alikuwa binti ya afisa wa polisi wa cheo cha juu ambaye alifika katika duka la Pasta Njora akiwa na hamaki, akamkamata mwendo wa saa nane na kabla ya saa kumi, alikuwa ameshtakiwa kwa wizi wa kipakatalishi na ambapo baada ya kukanusha mashtaka mahakama iliagiza atupwe rumande kwa kipindi cha siku 14 au atoe dhanama ya Sh100,000.

Wiki ya tatu akiwa katika rumande ya Viwandani kuna vijana wawili walioletwa na wakafahamiana na ambao anawatambua kama Kevoh na Njoroge.

“Waliniambia kuwa walikuwa wananifahamu kwa kuwa walikuwa na makao yao karibu na duka langu. Waliniambia nisiwe na wasiwasi kwa kuwa wangenisaidia. Waliagiza niwape namba ya kesi yangu na hakimu aliyekuwa akiishughulikia. Nilitii,” asema.

Wawili hao walikaa kwa rumande siku moja tu na wakatoka.

“Baada ya siku mbili, walikuja kunitembelea na ndipo waliniagiza kuwa nikirejeshwa mahakamani nikiri kuwa niliiba kompyuta hiyo ndogo. Nilifanya hivyo na sijui ni nini kilijiri kati yao na mahakama kwa kuwa nilishtukia tu nimeachiliwa. Hapo ndipo nilijua kwamba kufungwa huwa ni kwa hiari, ukijielewa, uhuru ni wako mahakamani bora tu ujue jinsi ya kuumiliki,” asema.

Wawili hao hatimaye walikiri kwake kuwa walikuwa majambazi sugu jijini na wakamsajili katika sakata ya wizi wa magari.

“Kazi yangu ya kwanza kufanya nao ilikuwa ya kuendesha gari la wizi hadi Tanzania na nikalipwa Sh65,000. Utamu wa pesa ukaniteka nyara na kabla sijajua nilikuwa nafanya nini, nikawa nimejipa kitambulisho na leseni bandia na ambazo nilitumia kukodisha magari na kuishia kuyauza,” asema.

Novemba 2007, Kevoh na Njioroge wakapigwa risasi na maafisa wa polisi.

“Niliponyoka mauti kwa kuwa mtoto wangu alikuwa akisumbuliwa na mwili na sikuandamana nao katika dili moja ya wizi ambayo ilitibuka na wakauawa,” asema.

Aliunda genge lingine la vijana wanne na ambao waligeuza mbinu ya wizi na wakakumbatia ule wa kimabavu wakiwa wamejihami kwa bunduki na bahati ya mtende tena ikamnusuru mauti ambapo wanne hao waliuawa na risasi za polisi mwaka wa 2008.

Akiwa na upweke wa ujambazi na tamaa ya pesa, mnamo Novemba 13, 2008, alijitokeza karibu na hoteli ya Hilton jijini Nairobi akiwa anaendesha gari la wizi na ambapo miongoni mwa raia alikuwemo mmoja wa wanawake ambao alikuwa ameibia gari hapo awali.

“Nilikuwa katika msongamano wa magari. Nilimwona huyo mwanamke akikimbia kwa gari langu akiwa anapiga usiahi. Nilijua mara moja nilikuwa katika hatari kuu. Nilijaribu kurudisha gari nyuma na nikagonga lililokuwa nyuma yangu. Nikajaribu kulisogeza mbele na nikagonga lililokuwa mbele yangu… Raia walinisakama na nikapewa kipigo cha kitutu kilichoishia kunakiliwa katika gazeti la Nation siku iliyofuata…Nilikuwa nimeingizwa shingo katika gurudumu na kumiminiwa petroli. Lakini kuna mwanamke alibishana akisema nisichomewe karibu na kibanda chake. Nilibururwa nikachomewe kwa barabara na ndipo polisi waliingia na wakafyatua risasi mbili juu. Kwa mara nyingine tena, nikanusurika mauti,” asema.

Lakini aliishia kushtakiwa na ambapo alihukumiwa miaka 22 gerezani lakini muujiza mwingine ukamwandama alipoachiliwa baada ya miaka 10.

“Hii ni baada ya ripoti za jela kunitetea kuwa nilikuwa nimebadili mienendo na hata nilikuwa nimesomea taaluma ya uchunganji iliyokuwa imenigeuza kuwa pasta katika gereza kuu la Kamiti,” asema.

Ni katika kipindi hicho cha kuhudumia kifungo chake alipookoka na alipotoka gerezani akakumbatiwa na Askofu Pius Muiru alioyempa ajira kama pasta wa kanisa lake la Maximum Miracle Centre.

You can share this post!

DIMBA NYANJANI: Karate ya ‘chini kwa chini’ ya Kenpo...

MBWEMBWE: Kwa mkwanja wa Sh35 milioni kuvumisha bidhaa za...