Habari Mseto

Pesa zaidi zitengewe matibabu ya saratani, magavana wasema

September 10th, 2019 1 min read

NA EVANS KIPKURA

MAGAVANA wawili kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa wameomba serikali kutenga pesa zaidi kugharimia matibabu ya saratani kwa familia maskini.

Alex Tolgos wa Elgeyo Marakwet na Jackson Mandago wa Uasin Gishu walisema kwamba gharama ya juu ya kutibu saratani imesababishia familia kadhaa umaskini na kuwaacha kwenye lindi la uchochole.

“Familia nyingi zimelazimika kuuza mali yao ili kugharimia matibabu ya jamaa zao. Hali hii imewazamisha kwenye lindi la umaskini,” akasema Bw Tolgos wakati ibada ya mazishi katika eneo la Kapsiliot, Uasin Gishu.

Gavana huyo aliongeza kwamba wakati umefika kwa serikali kuingilia kati na kuokoa watu ambao ugonjwa huo umechangia kufilisiwa kwa akiba yao.

“Kama mojawapo ya nguzo muhimu ya utawala wa serikali ya Jubilee, afya ni jambo ambalo linafaa kuchukuliwa kwa uzito unaostahiki na serikali,” akaongeza.

Kwa upande wake, Bw Mandago aliomba serikali kuondoa ada zote ambazo zinatozwa wakati vifaa vya matibabu vya kansa vinanunuliwa ili kaunti kadhaa zivinunue na kuvisambaza katika vituo vyao vyote vya kimatibabu.

Kulingana naye wagonjwa wengi hawawezi kugharimia matibabu ya kansa kutokana na bei ya juu ya vifaa vya matibabu.

“Gharama ya matibabu ya saratani ni ghali mno na watu wengi hawawezi kumudu gharama yake. Njia pekee ambayo serikali inaweza kuwasaidia wanaogua saratani ni kufutilia mbali ada zote kwenye vifaa na dawa zinazonunuliwa,” akasema Bw Mandago.

Naibu Gavana wa Elgeyo Marakwet Wesley Rotich naye alisema kaunti hiyo iko kwenye hatua za mwisho kufungua kituo kipya cha kutibu kansa chenye vifaa vya kisasa katika hospitali ya rufaa ya Iten.