Makala

PETER: Helb ifahamu wengi walionufaika bado hawana kazi

February 23rd, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

BODI ya Kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Helb) wiki hii imetangaza kuwa itaanza kutumia asasi za usalama kuwasaka watu ambao walinufaika na pesa zake, na kuwashurutisha kuzilipa.

Bodi hiyo ilisema zaidi ya watu 74,000 ambao wamepokea mikopo yake hawajakuwa wakilipa, ikishuku kuwa baadhi yao wako kazini lakini wameamua tu kutolipa.

Vilevile, Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema hawatasaza watu waliomaliza vyuo hata kama bado hawajaajiriwa katika kazi walizosomea, mradi wapo mahali wanapata mshahara mdogo, kama wahudumu wa MPESA na Airtel Money.

Nakubaliana na maamuzi ya serikali kuwa ni vyema kufuatilia pesa inazodai walionufaika na mikopo ya masomo, haswa ambao wako katika ajira zinazowafaidi maishani ama ambao wamefanikiwa katika biashara ama nyanja zingine za kiuchumi.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu ambaye amesaidika na pesa kama hizo kumwezesha kusoma kulipa deni hilo, ili kuwezesha maelfu ya wanafunzi wengine wanaotoka familia zisizojiweza kunufaika na kusoma bila changamoto.

Kwa kila hali, serikali iko sawa kufikia pesa hizo kwa watu kama hawa, ambao ijapokuwa walisaidika na hata baada ya masomo wakapata kazi na kuweza kujiimarisha katika maisha yao ya kiuchumi, hawaoni umuhimu wa kuzilipa kusaidia jamii kwa kuinua wengine. Watu kama hawa wanafaa kushurutishwa kuzilipa.

Hata hivyo, sikubaliani na serikali inaposema kuwa inapanga kuwafikia hata watu ambao licha ya kumaliza vyuo na kukaa kipindi cha muda nje bila kazi ama wakifanya kazi za malipo duni.

Ni ukweli ulio wazi kuwa idadi ya watu ambao wamemaliza masomo ya vyuo na vyuo vikuu lakini wakasalia kukaa nje bila ajira humu nchini ni ya wingi wa kushangaza.

Ualimu

Watu waliosomea ualimu pekee wanakaribia 300,000 hata bila kuongeza idadi ya watu waliosomea kozi zingine.

Ukweli ni kuwa kuna watu wengi ambao hawangependa kukaa na deni la bodi ya Helb lakini kutokana na hali ya kukosa ajira ama kuwa katika kazi ambazo zinawawezesha tu kuendesha maisha, wanakosa jambo la kufanya.

Maafisa katika bodi hiyo ni Wakenya ambao wanafahamu vyema matatizo ya ukosefu wa kazi ambayo ni jambo la kawaida nchini na hivyo hawawezi kuzibia macho suala hili.

Kwa hivyo, jambo linalojitokeza ni kuwa japo ni kweli bodi ya Helb inadai mabilioni ya pesa, kuna ukweli mwingine mchungu kuwa asilimia kubwa ya walionufaika na pesa zao hawakutimiza malengo, lengo kuu likiwa kupata kazi nzuri na kuendeleza maisha.