Makala

PETER KAMAU: 'Rabbi' anayedai kuwa na ufunguo wa kuingia mbinguni

April 22nd, 2019 3 min read

Na PHYLIS MUSASIA

JUMATATU ya Pasaka ni siku ambayo Wakristo husherehekea baada ya Yesu Kristo kushinda mauti.

Mjini Nakuru, yupo Bw Peter Joseph Kamau ambaye anapotembea taratibu akiwa na kanzu ya rangi ya mdalasini na fimbo nyeupe iliyochongwa kwa mfano wa ufunguo anaodai kuwa ufunguo rasmi wa kuingia mbinguni.

Mara nyingi utamuona akitembea mjini na kofia ya manjano iliyoshonwa na kuwachwa na kitambaa kirefu kinachoning’inia na kufunika sehemu yote ya mabega.

Kwake Bw Kamau, hiyo ni ishara tosha na inayoonyesha anahusiana na dini ya Legio Maria.

Nilipomkaribia “Rabbi” na kunyoosha mkono wangu ili tusalimiane, badala yake alishika ‘ufunguo wa mbinguni” na akauinua juu kisha akainamisha kichwa chake na kusema Amina. Ishara hiyo ilivutia idadi kubwa ya watu waliokuwepo sehemu hiyo ya Barclays mjini Nakuru, mara nikabaki kuzubaa nisielewe alichomaanisha na ishara hiyo.

Kwa kutaka kumjua na kumwelewa “Rabbi” nilianza kumuuliza kuhusu ishara aliyoifanya badala ya kunisalimu kwa mkono.

“Nilikuona ukinijia hata kabla hujanifikia. Nilifanya ishara hiyo ili kufungua mbingu na kutakasa moyo wako kabla ya kuzungumza na wewe. Sasa uko huru kuendelea,” akanieleza.

“Rabbi” alinieleza kuwa alinyakuwa jina na cheo chake baada ya kugundua kuwa mara nyingi alijikuta akifanya mambo mengi kwa njia isiokuwa ya kawaida.

Kwa mfano alisema alipokuwa mdogo alijitenga na watu na kukaa kanisani muda mwingi huku akijihusisha na kusoma bibilia miongoni mwa kazi nyingine kanisani.

“Sikuwa na hamu ya kukaa na mtu hata wazazi wangu, nilijitenga muda mwingi na kuamua kukaa kanisani hata wakati ambao haukuwa wa ibada. Nilijiona kuwa tofauti na ndipo nikajipa jina la Rabbi kumaanisha mwalimu,” akasema.

Bw Kamau alisema anaishi maisha ya kawaida kama watu wengine lakini tofauti yake ni kwamba matendo yake na tabia yanafanana sana na ya Yesu Kristo na pia ana uwezo wa kuzungumza na Mungu kwa njia ya moja kwa moja.

Kulingana naye, ana umri wa miaka 88 na wakati mmoja aliwahi kuwa mume na baba wa watoto tisa.

“Mke wangu aliaga dunia mwaka wa 1989 na pamoja tulikuwa tumejaliwa watoto tisa ingawa kwa sasa ni watatu tu ambao wako hai,” akasema.

Kazi yake alisema ni kutoa mafundisho ya Biblia kwa watumishi wa Mungu na waumini wa makanisa mbalimbali. Yeye huzunguka kwenye makanisa kadha wa kadha akiwafundisha watu kuhusiana na maandiko yalivyo kwenye Biblia.

Alisema alipata upako na kuianza kazi hii alipokuwa na umri wa miaka minne na hapo ndipo aligundua kwamba yeye ni mtu tofauti na watu wengine.

“Nilipokuwa mdogo sikuwa kama mtoto wa kawaida wa kucheza na kufanya mzaha kama watoto wengine, nilijitenga na mara nyinyi nilipenda sana kukaa kanisani. Tulishiriki kanisa la P.C.E.A ambapo nilikaa kwa muda wa miaka 30,” akasema.

Baadaye alijiungana na kanisa la Legio Maria ambalo amehudumu kwa muda wa zaidi ya miaka 40.

Kwa sasa, Kamau alisema anaishi pekee yake na kwamba yeye hula chakula ambacho amekiandaa yeye mwenyewe.

“Siri ya kuishi miaka mingi ni kujipikia na kula chakula ambacho umekipika mwenyewe,” akaongeza.

Mkewe alipoaga dunia, aliishi peke yake kwa muda wa miaka 30, lakini hivi maajuzi alisema alijiwa na ndoto iliyomwonyesha binti wawili ambapo mmoja ni wa umri wa miaka 30 ambaye anatazamia kumuoa.

Kulingana naye, tayari amemweleza binti huyo kuhusiana na ndoto aliyosema ilitoka kwa mwenyezi Mungu lakini la kushangaza ni kwamba hakumweleza binti huyo ikiwa ni yeye ambaye anahusishwa kwenye ndoto aliyoota Kamau.

“Siogopi kumweleza kwamba ni yeye ambaye ndiye atakuwa mke wangu baada ya kuonyeshwa na Mungu kwenye ndoto, ila tu, nahisi kwamba wakati mwafaka haujafika,” akasema.

Hata hivyo, alisema anapaswa kuweka mikakati yote kabla ya kumweleza binti huyo kwani anapanga kwenda kwao kujitambulisha na kulipa mahari kabla ya kufunga naye pingu za maisha.

Baadaye atamwendea binti wa pili ambaye hajaweza kuonyeshwa sura yake na Mungu, lakini yuko na matumaini kwamba hilo litatimia hivi karibuni.

Alisema binti hawa wawili wako kwenye kaunti ya Nakuru na kwamba ndoto iliyomjia ilidhihirisha kwamba wanaishi maisha ya kibikra na isiojihusisha na mambo mabaya ya dunia hii.

“Wake zangu wako mahali katika mji huu na wanafanya bidii sana. Hivi karibuni watajitokeza na watakuwa wangu wa maisha. Najua watanipenda kwa dhati kwani tayari Mungu amenionyesha hayo yote,” akaeleza Bw Kamau huku akitabasamu.

Bw Kamau alisema yuko tayari kupata watoto wengi na hataruhusu wake zake kupanga uzazi kwani kulingana naye mwanamke yeyote anayepanga uzazi anafanya dhambi.

Mwanamke anafaa kutumika kama chombo cha mwanamume na akijihusisha na upangaji uzazi hilo litakuwa kama kosa la kuuwa watoto kama sio kufunga utumbo wake.

“Sina wasiwasi kwamba nitakapopata watoto na wake zangu wawili nitakuwa na shida ya pesa, tayari Mungu ameniagizia hela na mali ya kutosha na hakuna yeyote kati yao atakaye angaika,” akajigamba.

Kamau alisema amewahi kusafiri katika nchi ya Congo ambapo alielekezwa kwenye ndoto kwenda kupeana mafunzo ya Bibilia. Alikaa huko kwa muda wa miezi miwili kabla ya kurejea nchini Kenya.

“Niliabiri basi hadi Malaba na nikaingia nchi ya Uganda, kutoka hapo nikasafiri hadi Zaire ambapo nilielekezwa na Mungu. Kazi yote ilienda sawa na nilipomaliza shughuli nikarudi nyumbani,” akaeleza.