Habari

Peter Ndegwa atangazwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom

October 24th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

PETER Ndegwa ametangazwa Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa kampuni ya Safaricom; nafasi ambayo imekuwa ikishikiliwa na Michael Joseph kama kaimu tangu kufariki kwa Bob Collymore Julai 1, 2019.

“Bodi ya wakurugenzi ya Safaricom Plc imeamua kumteua Peter Ndegwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji kuanzia Aprili 1, 2020,” amesema mwenyekiti wa Safaricom Bw Nicholas Ng’ang’a kwenye taarifa Alhamisi akliongeza kwamba uamuzi huo uliafikiwa kwa kuzingatia tajriba na ujuzi wa Ndegwa.

Hatua hii inajiri siku moja tu baada ya Joseph kuambia wanahabari Jumatano kwamba uamuzi ulikuwa haujaafikiwa.

Ndegwa alikuwa Mwafrika wa kwanza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni kubwa ya bia ya Diageo; hasa operesheni za Uropa na Urusi kuanzia Julai 2018 kufikia sasa. Ataanza kazi rasmi Safaricom kuanzia Aprili 2020.

Awali aliwahi kuwa afisa mkuu wa kampuni ya Guinness Nigeria Breweries Plc, ambayo ni tawi la Diageo.

Aidha, Ndegwa alijiunga na kampuni ya East African Breweries Limited mnamo Januari 2004 na akawa hapo kama Mkurugenzi wa Fedha na alikuwa amewahi kufanya kazi katika PricewaterhouseCoopers.

Baina ya mwaka 2011 na 2015, alikuwa Meneja Mkurugenzi wa Guinness Ghana Breweries.

Awali duru zilikuwa zimesema kwamba Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ilikuwa imekosa kukubaliana kuhusu uteuzi wa afisa mkuu mpya kuchukua nafasi ya Boby Collymore aliyefariki miezi mitatu iliyopita.

Duru zilikuwa zimesema kuwa wanachama wa bodi hiyo waliokutana Jumanne usiku walikuwa wamekosa kuafikiana kuhusu suala hilo.

Bw Joseph aliteuliwa kushikilia wadhifa wa huo kwa muda kutoa nafasi ya kuteuliwa kwa mtu atakayejaza nafasi rasmi.

Kwa muda mrefu, kumekuwepo na madai kwamba mshikilizi wa cheo hicho ulicheleweshwa kutokana na mivutano ya kimasilahi katika kampuni hiyo huku ikidaiwa kuwa serikali ilitaka kuwa na usemi mkubwa ikizingatiwa kuwa ina asilimia 35 ya hisa katika kampuni hiyo.

“Mkutano uliendelea hadi Jumanne usiku, siku ya kuamkia maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa kampuni hii. Wasimamizi wakuu walihisi kuwa nafasi ya Afisa Mkuu Mtendaji inapasa kujazwa, lakini hiyo haikufanyika,” afisa mmoja wa cheo cha juu katika Safaricom alinukuliwa akisema.

Vilevile, ilidaiwa kuwa wanachama wa bodi hiyo walikuwa wamegawanyika kuwili kuhusu iwapo nafasi hiyo ilifaa kupewa Mkenya au raia wa kigeni.

Duru zilisema kuwa mwenyekiti wa muda mrefu wa bodi hiyo Nicholas Ng’ang’a alikuwa miongoni mwa wale waliotaka nafasi hiyo ijazwe na Mkenya.

Mnamo Aprili 2019 Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru alisema hivi: “Hakuna kitu spesheli katika uendeshaji wa kampuni za mawasiliano, naamini Mkenya pia anaweza kuendesha Safaricom kama Afisa Mkuu Mtendaji.”

Kauli hiyo iliendeleza fununu kwamba serikali inataka kuingilia kati shughuli hiyo kuhakikisha kuwa cheo hicho kinashikilia na Mkenya.

Bw Ng’ang’a ni mwakilishi wa serikali katika bodi hiyo na amefanya mikutano mingi na maafisa wa serikali pamoja na kampuni ya Vodafone kutoka Uingereza, ambayo ndiyo ina hisa nyingi zaidi katika kampuni hiyo.

Hata hivyo, Safaricom imepuuzilia madai kuwa serikali ilitaka wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji ushikiliwe na Mkenya.

“Serikali inamiliki asilimia 35 ya hisa katika kampuni hii na ina haki ya kutoa kauli, maoni na hata mapendekezo yake. Lakini kufikia sasa haijaingilia mchakato wa uteuzi wa Afisa Mkuu,” Bw Joseph akasema Jumatano wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Safaricom nchini.

Afisa mwingine wa Safaricom alinukuliw akisema kampuni hiyo huendesha masuala yake kwa mipango na itatoa tangazo hilo wakati ufaao. “Safaricom hua haifanyima mambo yake bila mipango,’ akasema.

Kufuatia mvutano kuhusu suala hilo, sasa inasemekana kuwa serikali imejiondoa katika suala hilo na kuiachia bodi ya wasimamizi na kampuni ya Vodafone.

Safaricom imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) na ina zaidi ya wateja 30 milioni na huzalisha mapato ya kima cha Sh200 bilioni kila mwaka.

Wale ambao walikuwa wakipigiwa upatu kupata kazi hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Kiufundi katika Safaricom Joseph Ogutu ambaye anakaribia kustaafu, Mkurugenzi wa Masuala ya Biashara katika kampuni hiyo Silvia Mulinge na Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Nzioka Waita.

Aidha, duru zinasema raia mmoja wa Ugiriki anayehudumu katika mojawapo ya matawi ya Vodafone katika Mataifa ya Mashariki ya Mbali na Uropa pia alikuwa ameorodheshwa kwa kazi hiyo.