PETER NGARE: Tusihadaike eti ‘kazi ni kazi’ wala pesa za bure

PETER NGARE: Tusihadaike eti ‘kazi ni kazi’ wala pesa za bure

NA PETER NGARE

WANASIASA ni watu wajanja sana. Ujanja huu wao huwa unasukumizwa na ubinafsi ambao hutawala kila neno wanalotamka ama hatua wanazochukua.

Wanasiasa hawa huwa wamejaaliwa ama kujifunza mbinu za kuteka akili za umma, hasa za maskini, sawa na wafanyavyo wahubiri matapeli.

Wanasiasa huwa wanatapeli wananchi kura zao nao wahubiri wapotovu huibia waumini kidogo walicho nacho.

Mbinu ambazo matapeli hawa wote hutumia ni kutawala akili za walio na matatizo mbalimbali kwa kuwaonyesha kuwa wao ndio wenye suluhu kwa masaibu yanayowakumba.

Wanajua kutumia maneno matamu matamu na laini kama ini kuwapumbaza wanaolengwa, na kufumba na kufumbua wanahepa na kura ama mali zao.

Kipindi hiki ambapo Kenya inaelekea kwenye uchaguzi mwaka ujao, wanasiasa wakuu hasa Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaendeleza tabia za kitapeli.

Wote wawili wameweka nguvu zao kwa watu ambao wanahangaika kwa matatizo ya kiuchumi na wanajidai kuwa ndio wenye dawa ya umaskini.

Lakini ukiwasikiza vizuri na kuwatazama hawana lolote, ila wanachotaka ni wapigiwe kura kisha waponyoke tuwaone miaka mitano ijayo wakija na mbinu zizo hizo za kitapeli kuomba kura tena.

Mfano mzuri ni kauli mbiu ya Dkt Ruto kwa ‘mahasla’ kuwa ‘kazi ni kazi’. Hii ni kauli potovu kwani Naibu Rais anafahamu fika kuwa huu ni udanganyifu unaolenga akili za watu waliokadamizwa kiuchumi, na wako tayari kunasa makopo aina yoyote wanayorushiwa.

Dkt Ruto na washirika wake wanajua kuna kazi nyingi ambazo watu wanafanya kwa kukosa namna ama kupoteza matumaini maishani. Hizi ni kazi ambazo yeye mwenyewe hawezi akazifanya wala kutaka mtoto wake azifanye.

Kwa mfano hakuna mtu angependa kusukuma wilibaro kwenye jua kila siku kama angeweza kupata kazi nyingine yenye mapato ya juu na isiyo ya kuadhibu kama hiyo.

Kama kweli Dkt Ruto anataka kusaidia watu anaodai ana maono mema kuwahusu, basi angetoa mpango mahsusi wa kuhakikisha vijana wanye digrii na diploma wanaofanya kazi za vibarua wamesaidiwa kufanya kazi za taaluma walizosomea chuoni.

Kama kweli angetaka kuinua mama mboga angetoa mikakati ya kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi, kuwaondolea mabroka, kupunguza ada wanazolipa na kuwalinda dhidi ya kuhangaishwa na askari wa kaunti.

Kwa upande wake Bw Odinga anadai atawapa maskini Sh6,000 kila mwezi kana kwamba yeye ni ‘Papa Krismasi’ awape watu vya bure.

Bw Odinga na washauri wake wanapasa kujua kuwa hakuna mwanadamu aliye na akili timamu na afya nzuri anaweza kujivunia kupewa mapeni bila kuyafanyia kazi, labda awe mvivu wa kulaaniwa. Hadhi ya binadamu inatokana na kazi anayofanya, pesa huwa ni matokeo tu.

Hivyo, kupanga kila mwezi kuwa utawapatia watu pesa bure bure ni sawa na kudhalilisha ubinadamu wa walengwa. Badala yake ‘Baba’ angebuni mikakati ya kuimarisha uchumi ili kusisimua ukuaji utakaosaidia kubuni nafasi zaidi za kazi.

Hivyo basi, Wakenya wanapasa kuzinduka na kufahamu kuwa wanatapeliwa kwa ajili ya kura zao mwaka ujao na wanapasa wakatae kupumbazwa kwa ahadi za pesa nane.

Badala ya kudai kuelezwa mipango mahsusi na itakavyotekelezwa kuboresha hadi ya maisha yao, wala sio kuambiwa wafanye kazi yoyote hata kama haina heshima, ama kwamba watapewa pesa bila jasho.

Hii ni kauli potovu kwani Naibu Rais anafahamu fika kuwa huu ni udanganyifu unaolenga akili za watu waliokadamizwa kiuchumi.

Mwandishi ni Mhariri Mkuu wa gazeti la Taifa Leo pngare@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Makali ya janga la ukame yawasukuma baadhi ya wanaume...

JUMA NAMLOLA: Ni kazi bure kuahidi kuimarisha uchumi bila...

T L