Michezo

Phil Jones kukosa kampeni zilizosalia za Manchester United kwenye Europa League

August 11th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Phil Jones wa Manchester United hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Ole Gunnar Solskjaer kwenye michuano yote iliyosalia ya Europa League msimu huu kwa sababu ya jeraha la goti.

Mara ya mwisho kwa sogora huyo mwenye umri wa miaka 28 kuwajibishwa na Man-United ni katika gozi la Kombe la FA dhidi ya Tranmere mnamo Januari 26, 2020.

“Jones amekuwa akijifanyia mazoezi mepesi ya nyumbani tangu Juni 2020. Anaendelea vizuri na atakuwa sehemu ya kampeni za muhula ujao,” akasema Solskjaer.

Baada ya kuwadengua FC Copenhagen ya Denmark kwenye robo-fainali ya Europa League mnamo Agosti 10, 2020, Man-United watavaana sasa na mshindi wa robo-fainali nyingine itakayowakutanisha Wolves ya Uingereza na Sevilla ya Uhispania mnamo Agosti 11, 2020.

Mechi zote za robo-fainali, nusu-fainali na fainali ya Europa League zitachezewa katika majiji ya Dusseldorf, Gelsenkirchen, Duisburg na Cologne nchini Ujerumani.

Baada ya robo-fainali kusakatwa kati ya Agosti 10-11, mechi za nusu-fainali zitatandazwa Agosti 16-17 kabla ya fainali kuandaliwa Agosti 21, siku mbili kabla ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kunogeshwa jijini Lisbon, Ureno.

Jones amechezeshwa na Man-United katika mechi nane pekee msimu huu wa 2019-20. Beki mwingine ambaye atakosa kuwa sehemu ya kikosi cha Man-United katika kampeni zilizosalia za Europa League msimu huu ni Axel Tuanzebe anayeuguza jeraha la kifundo cha mguu.