Michezo

Phil Neville asema Guardiola amemshauri aanze kumakinikia soka ya klabu badala ya timu ya taifa

June 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Uingereza, Phil Neville, amesema kwamba mkufunzi Pep Guardiola wa Manchester City amemshauri kuanza kumakinikia soka ya klabu badala ya timu ya taifa.

Neville anatarajiwa kuagana rasmi na timu ya taifa ya Uingereza almaarufu ‘Lionesses’ mwishoni mwa msimu a 2021. Kufikia wakati huo, atakuwa amedhibiti mikoba ya kikosi hicho kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu.

“Nilizungumza na Guardiola akanishauri hizi nguvu nilizonazo katika kunoa klabu badala ya timu ya taifa ambayo huwajibishwa baada ya vipindi virefu vya muda,” akatanguliza Neville.

“Makocha wa haiba kubwa kufu ya Guardiola wana uwezo wa kumshawishi yeyote. Nami nilishawishika na kuona mantiki katika alichonishauri,” akasema.

Guardiola ambaye ni mkufunzi wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich anajivunia kutia kapuni jumla ya mataji 30 akiwa kocha. Mbali na kushindia Barcelona makombe mawili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), haya ni mataji aliyoyanyua katika soka ya Uhispania, Ujerumani na Uingereza.

Neville ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Manchester United, Everton na timu ya taifa ya Uingereza, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa Lionesses mnamo Januari 2018.

Chini ya ukufunzi wake, Uingereza walitawazwa mabingwa wa SheBelieves Cup kisha wakaambulia nafasi ya nne kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 2019. Hata hivyo, wamepoteza jumla ya mechi saba kati ya 11 zilizopita tangu wawazidi maarifa Norway kwenye robo-fainali za Kombe la Dunia.

“Japo hakuna presha ya kunoa timu ya taifa, mtu hujihisi mpweke mara kwa mara wachezaji wanapolazimika kuondoka kambini mwa kurejea katika klabu zao. Jambo hilo humwacha kocha wa timu ya taifa bila ushawishi wala usemi wowote,” akasema Neville, 43.

“Kwa sasa nina takriban miezi 12 zaidi ili kudhibiti mikoba ya Lionesses. Ni matarajio yangu kwamba nitapata fursa ya kuwa kocha wa klabu au hata kocha msaidizi katika kikosi cha haiba kubwa Uingereza au taifa jingine,” akaongeza.

Neville alitarajiwa kuongoza kikosi chake cha Lionesses kwa Michezo ya Olimpiki iliyoahirishwa hadi 2021 kabla ya kuwaongoza vipusa wake kutwaa ubingwa wa Euro mnamo Julai 2022 mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Hadi alipopokezwa mikoba ya Lionesses, Neville alikuwa kocha wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 kambini mwa Man-United na Uingereza kabla ya kutua Uhispania kuwa msaidizi wa kaka yake Gary kambini mwa Valencia.

Wawili hao wana dada, Tracey, aliyewahi kuongoza timu ya taifa ya Uingereza kutia kapuni nishani ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyoandaliwa jijini Gold Coast, Australia mnamo 2018.