Habari

PICHA: Mzozo wazua kubomolewa kwa nyumba 20 Railways, Nairobi

February 20th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

MZOZO wa usimamizi wa mali ya mamilioni ya watu waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Reli, Nairobi ulifikia kilele Jumatano na kusababisha ubomoaji wa zaidi ya nyumba 20 za kuishi na nyingine za kibiashara, familia zikiachwa bila makao.

Familia ambazo zilikuwa zikiishi katika nyumba zilizokuwa ndani ya shamba hilo ziliamkia matukio ya kutamausha, wakati kikundi cha zaidi ya vijana 50 kiliwavamia, kubomoa milango ya nyumba na kuanza kutupa vitu nje.

Wakazi walisema kuwa katika harakati hizo walipoteza mali na pesa, wakisema wahuni waliofika kuwafurusha walitumia nguvu na kuharibu mali yao.

Tingatinga liliamkia kubomoa makazi ya wapangaji eneo la Railways, Nairobi Februari 20, 2019. Picha/ Peter Mburu

Wakati Taifa Leo Dijitali ilifika eneo hilo, karibu na bustani ya Uhuru Park, mali ya watu yalikuwa yametapakaa nje ya nyumba zao, huku kikundi cha vijana wakiendelea kubomoa.

Tinga la kutekeleza ubomoaji baadaye liliwasili na kuangusha nyumba hizo, katika matukio yaliyowaacha wakazi bila matumaini.

“Walituvamia alfajiri hata kabla ya saa kumi na mbili, niliamka na kupata watu zaidi ya 10 ndani ya nyumba ambao walikuwa wakitoa vitu nje na kuwafurusha watu. Nimepoteza kipakatalishi na Sh12,000 ilhali nimekuwa nikiishi hapa kwa njia ya haki,” akasema Carilus Atwala, mkazi aliyeathirika.

Mali ya wapangaji yatapakaa baada ya ubomoaji. Picha/ Peter Mburu

Wakazi wengine walilalamika kuwa walibaki bila makao ilhali wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa hadi zaidi ya miaka 20.

Mzozo huo unahusisha shamba la ukubwa wa ekari 18 linalopakana na bustani ya Uhuru Park, ambalo zaidi ya wafanyakazi 9,000 wastaafu wa shirika la Reli wanamiliki, baada ya kufidiwa na shirika hilo liliposhindwa kuwalipa pesa za uzeeni.

Walipewa shamba hilo, pamoja na mengine, mnamo 2006 na tangu wakati huo wamekuwa wakimiliki na kukodesha, na hata kuuza mengine.

Mary Adhiambo ambaye alipoteza mali na Sh30,000 pesa taslimu kwenye ubomoaji huo. Picha/ Peter Mburu

Klabu ya Nairobi Railway ilikuwa ikikusanya pesa wanazolipa wakazi na wafanyabiashara na kuwapa wazee hao kupitia muungano wao wa KRSRBS, japo viongozi wa muungano huo walidai kuwa kwa miaka minne sasa hawajakuwa wakifikiwa na pesa hizo.

Walidai watu fulani wamekuwa wakizitia mfukoni huku wengi wao ambao ni wazee wakongwe wakiendelea kuteseka.

“Baadhi ya watu katika klabu hii wamekuwa wakichukua pesa zetu kama ni zao na hivyo hawatulipi. Tunafaa kuwa tukipokea zaidi ya Sh2 milioni kila mwezi, japo pesa hizo zinapotelea katika mifuko ya watu,” akasema Bw Johnson Miano, mwenyekiti wa wastaafu hao.

Sehemu ya burudani ya watoto pia haikusazwa. Picha/ Peter Mburu

Bw Miano alisema mahakama ilikuwa imeamrisha wapangaji wa nyumba za biashara na za kuishi kuelewana na wastaafu hao ili wawe wakiwalipa kodi moja kwa moja, lakini walipokosa kufanya hivyo korti ikaamrisha nyumba hizo zibomolewe.

Lakini Meneja Mkuu wa klabu hiyo Eliphas Wesangula alikosoa hatua ya ubomoaji huo kutekelezwa, akisema ni kinyume na sheria kwani kuna kesi inayoendelea kortini kwa sasa nab ado hawajaruhusiwa kutetea upande wao.

Wafanyakazi wa mashirika mbalimbali walifungiwa nje wakati wa ubomoaji huo. Picha/ Peter Mburu

“Klabu haikufahamishwa kuwa korti imeruhusu utekelezaji wa hasara hii. Kile wamefanya leo ni haramu,” akasema Bw Wesangula.

Meneja huyo alikiri kuwa korti ilikuwa imewapa fursa ya kufanya mazungumzo na kuelewana namna pesa za kodi zingewafikia wazee hao moja kwa moja, japo akasema wamekosa subira na kutekeleza ubomoaji hata kabla ya kesi iliyopo kortini kuisha.

Alisema mawakili wa klabu hiyo wanatarajiwa kufika kortini Machi 20 na Aprili 11 na 15 kueleza upande wao.

Sehemu ya kidimbwi cha kuogelea pia kiliharibiwa. Picha/ Peter Mburu

Lakini hata pande zote mbili zikizidi kuvutana, wakazi wamesalia bila msaada, wengi wao wakishangaa watakapoenda kuanzia maisha.

“Nimeishi hapa kwa zaidi ya miaka saba na sasa nimefurushwa bila kujua ninapoanzia. Nina mtoto wangu ambaye ni mgonjwa na pesa za kumlipia hospitali zimeibiwa na wahuni waliokuja kutufurusha, nimepoteza Sh30,000,” akasema Bi Mary Adhiambo.