HabariSiasa

PICHA: Simanzi na vilio Sharon Otieno akizikwa

October 19th, 2018 1 min read

NA RUTH MBULA

WINGU la simanzi, lilitanda Alhamisi mwili wa Sharon Otieno, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo aliyeuawa mwezi mmoja na nusu uliopita, ulipoondolewa mochari na kupelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuzikwa.

Mazishi ya Sharon yanafanyika Ijumaa. Watu kadhaa, akiwemo mama yake Melida Auma, walizirai mwili ulipofikishwa nyumbani kutoka mochari.

Kwa zaidi ya saa moja, alikuwa amepoteza fahamu huku jamaa wakijaribu kumpa huduma ya kwanza. Waombolezaji hao walivumilia mvua kubwa kumpa heshima za mwisho binti yao.

Wakazi watazama mwili wa Sharon Otieno Ijumaa Oktoba 19, 2018 katika kijiji cha Magare, Kaunti ya Homa Bay. Picha/ Ruth Mbula

Babake Sharon, Douglas Otieno alijipa nguvu, alikataa kuzungumza na wanahabari na kutikisa kichwa waandishi wa Taifa Leo walipomkaribia.

Mwili wa Sharon uliondolewa mochari ya hospitali ya Med25 International-Kenya, Mbita saa tano mchana.

Akiwa mochari Bw Otieno alisema kifo cha binti yake kiliathiri familia yake sana. Alisema hakuna maneno yanayoweza kueleza huzuni yao, hakuna kilio kinachoweza kuponya mioyo yao na hakuna machozi yanayoweza kufidia binti yao.

Babaye Sharon, Bw Douglas Otieno asoma gazeti la Daily Nation lililochapisha habari ya kifo cha bintiye. Kushoto ni mkewe Bi Melida Auma wakati wa mazishi ya binti yao Oktoba 19, 2018. Picha/ Ruth Mbula

Mwili wa Sharon ulifikishwa nyumbani kwa wazazi wake ambapo utakesha kulingana na desturi za jamii ya Waluo. Atazikwa kando na kaburi ya mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa.

Bw Otieno alisema waliamua kuzika mwili baada ya kuamini kuwa haki itatendeka.

“Tumeona washukiwa waliohusishwa na mauaji yake wakifikishwa kortini. Tuko na furaha na uchunguzi kufikia sasa na tunaamini wauaji watawajibikia uhalifu wao,” alisema.

Majirani wampa pole mamaye Sharon Bi Melida Auma wakati wa mazishi ya bintiye. Picha/ Ruth Mbula

Familia ilikuwa imeapa kutozika mwili wa Sharon hadi wauaji wake wakamatwe na kushtakiwa.

Washukiwa wakuu miongoni mwao gavana wa Migori Okoth Obado wamezuiliwa rumande wakisubiri uamuzi wa ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Bw Obado na msaidizi wake Michael Juma Oyamo na karani wa bunge la Kaunti ya Migori Casper Obiero, wameshtakiwa kwa mauaji ya Sharon na mtoto wake ambaye alikuwa bado hajazaliwa.

Mapema wiki hii kesi zao ziliunganishwa. Obado amekuwa rumande kwa wiki tatu sasa. Alilazwa katika hospitali Kuu ya Kenyatta baada ya kuugua.