Habari za Kitaifa

Picha za CCTV zaonyesha dakika za mwisho za Dkt Kiptoo kabla apatikane ameuawa Nakuru

January 19th, 2024 2 min read

NA MERCY KOSKEI

PICHA mpya za kamera za CCTV zikionyesha dakika za mwisho za Dkt Laban Kiptoo aliyeuawa kwa njia tata zimepatikana huku mashahidi wakuu wakielezea jinsi walivyotangamana na marehemu.

Haya yanajiri baada ya wapelelezi wa kuchunguza mauaji, kutoka Nairobi, kuvalia njuga uchunguzi huo.

Mwili wa Dkt Kiptoo ulipatikana kwenye mtaro katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru wiki moja iliyopita.

Picha hizo za CCTV ambazo Taifa Leo ilifaulu kuziona, zilionyesha marehemu akitembea pekee yake akielekea hospitalini mwendo wa saa sita na dakika 21 (12: 21) Jumamosi usiku akitoka kilabu kimoja cha burudani eneo la London.

Baada ya kumkataa mwendeshaji mmoja wa bodaboda, alielekea katika duka moja la mvinyo lililokuwa limefungwa, kisha akaabiri boda boda nyingine.

Mlinzi katika duka hilo, Emmanuel Cheruiyot alisema kuwa alimshauri Dkt Kiptoo kutumia pikipiki kwa sababu eneo hilo huwa hatari nyakati za usiku.

“Aliondoka na kuenda kando ya barabara baada ya kugundua kuwa duka la mvinyo lilikuwa limefungwa. Mtu wa bodaboda alikuwa wakajadiliana na kukosa kuelewana kuhusu nauli na akaondoka. Dakika chache baadaye nilimwona akiabiri pikipiki nyingine na kuondoka. Sikushughulika kwani sikumjua,” Bw Cheruiyot akasema.

Taifa Leo pia ilimpata Bw Domic Yegon, mwendeshaji bodaboda aliyemfikisha mwendazake mahala alikuwa akienda.

Kwenye mahojiano, Bw Yegon alieleza jinsi Dkt Kiptoo, awali, alikataa huduma zake nje ya klabu moja ambako alikuwa akiburudika na watu wengine.

Alipokuwa akielekea nyumbani baadaye, alishangaa pale mwanamume mmoja aliyekuwa akitembea karibu na mzunguko wa barabara wa ASK alipomwonyesha ishara ya kumtaka asimame.

Mwanamume huyo alikuwa ni Dkt Kiptoo.

“Aliomba apelekwe katika kitengo cha kuwahudumia watoto cha Margaret Kenyatta ndani ya hospitali hiyo. Walinzi hawakutusimamisha kutuuliza tulikokuwa tukienda. Aliomba nimshushe karibu na kitengo cha akina mama kujifungulia, akisema alikuwa salama. Alikuwa mlevi lakini aliweza kulipa nauli na kuondoka,” Bw Yegon akasema.

“Nilimwacha akielekea kitengo cha akina mama kujifungulia. Sikufahamu ikiwa alienda kwingineko. Baadaye nilishangaa kuwa mteja huyo alikufa na nikatakiwa kuandikisha taarifa na DCI,” alieleza.

Dkt Stephen Obiero, ambaye ni rafiki wa karibu wa Dkt Kiptoo, alimtaja marehemu kama mchapakazi na mtu aliyejitolea katika taaluma yake ya afya ya uzazi.

Wawili hao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka saba tangu wakiwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Dkt Obiero alisisitiza kuwa rafiki yake alikuwa mtu mwerevu zaidi na wote wawili walikuwa mashabiki wa kandanda.

“Alikuwa mwanafunzi mwerevu darasani, alifahamu mbinu ya kujiandaa kwa mitihani. Dkt Kiptoo alikuwa miongoni mwa wanafunzi watano bora katika darasa letu. Baada ya kufuzu, tulikutana katika katika taasisi moja kwa mafunzo ya utendakazi. Hakusubiri kuajiriwa na Wizara ya Afya,” Dkt Obiero akaeleza.