Makala

Picha za Gladys Shollei akifurahia maisha baada ya kutalikiana na mumewe zasambaa mitandaoni

January 25th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

PICHA za aliyekuwa Msajili wa Idara ya Mahakama Gladys Boss Shollei zimeibua gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kusambazwa mno mnamo Ijumaa, Januari 24.

Mwakilishi huyo mwanamke katika Kaunti ya Uasin Gishu alizua mjadala mkali kutokana na picha hizo zilizoonyesha akimshika na kumkumbatia mwanamume Mzungu kwa namna inayoashiria uhusiano wa kimapenzi kati yao.

Wanamitandao walishindwa kujizuia hasa ikizingatiwa kwamba picha hizo zilijiri siku chache tu baada ya mwanasiasa huyo kuandika barua ya kuvutia hisia kwa aliyekuwa mumewe kufuatia talaka yao iliyovuma sana mitandaoni.

Kama kutia msumari moto kwenye kidonda, Sam alisonga upesi na kufunga ndoa na aliyekuwa mfanyakazi wake, Faith Ronoh kutoka Chepkorio, Elgeyo Marakwet, siku mbili tu baada ya ndoa yake ya miaka 20 na Gladys kuvunjwa rasmi.

Hata kabla ya kupona makovu ya utengano, Sam na Faith walirasimisha uhusiano wao mnamo Ijumaa, Januari 10 katika sherehe ya kitamaduni inayofahamika kama Koito.

Hatua hiyo ilimtonesha kidonda Gladys huku wafuasi wake na wanamitandao wakifurika kumfariji.

Hata hivyo, masaibu yake ya ndoa yalichukua mkondo wa kusisimua ambapo kwa mara ya kwanza, wanawake waliungana pamoja bila kujali kabila, umri au hadhi yao katika jamii dhidi ya wanaume kuhusu hatua hiyo.

Mjadala mkali uliibuka huku kukiwa na hisia changamano ambapo idadi kubwa ya wanaume walimkashifu huku wanawake wakiwazima na kumpongeza Gladys kwa kusonga mbele na maisha kama bosi sawa na jina lake na kutoruhusu talaka hiyo kumtamausha.

Mbunge wa Suba Kusini Millie Odhiambo alijitosa katika mtandao wa kijamii wa Facebook akiwa na ujumbe wa pongezi kwa mwakilishi huyo.

“Kongole mwenzangu,” aliandika Millie.

Hatungeweza kuthibitisha uhusiano kati ya Gladys na mwanamme huyo huku tukisubiri kauli kutoka kwa kiongozi huyo.

Ndoa ya miaka 20 kati ya Gladys na Sam Shollei ilivunjiliwa mbali katika Korti ya Milimani mnamo Januari 8.

Hakimu Mkuu PN Gesora, aliyeruhusu talaka hiyo kwa “misingi ya ukatili” aliitaja ndoa hiyo kama “iliyovunjika na haiwezi kurekebishwa.”

Kesi hiyo ya talaka iliripotiwa kuwasilishwa na Sam mnamo Septemba 6, 2019.

Alieleza korti kwamba wamekuwa wakiishi kando na Gladys kwa miaka minne.