Michezo

Pigo Barcelona na Bayern baada ya Fati na Kimmich kupata majeraha

November 11th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI matata wa Barcelona, Ansu Fati, sasa atakuwa nje kwa miezi minne baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 18 alifanyiwa upasuaji baada ya kupata jeraha wakati akicheza dhidi ya Real Betis mnao Novemba 8, 2020.

Barcelona waliibuka washindi wa mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyochezewa ugani Camp Nou kwa mabao 5-2.

Hadi alipopata jeraha hilo ambalo litamkosesha zaidi ya mechi 20 zijazo za Barcelona katika mapambano yote, Fati alikuwa amechezea kikosi hicho cha kocha Ronald Koeman mara 10 na akafunga mabao matano na kuchangia mengine mawili.

Nyota huyo mzawa wa Guinea-Bissau na raia wa Uhispania alivunja rekodi ya kitaifa ya Uhispania kwa kuwa mwanasoka mchanga zaidi kufunga bao ndani ya jezi za timu ya taifa alipocheka na nyavu za Ukraine mnamo Septemba akiwa na umri wa miaka 17 na siku 311.

Mbali na Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, vikosi vingine ambavyo vimepata pigo ni Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani ambavyo kwa sasa vitakosa maarifa ya kiungo Joshua Kimmich.

Kimmich, 25, atakuwa nje hadi Januari 2021 baada ya kufanyiwa pia upasuaji wa goti kutokana na jeraha alilolipata katika gozi la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) dhidi ya Borussia Dortmund mnamo Novemba 7, 2020. Bayern waliibuka washindi wa mechi hiyo kwa mabao 3-2 uwanjani Allianz Arena na kupaa hadi kileleni mwa jedwali la Bundesliga.

Kimmich atakosa sasa mechi zijazo za UEFA Nations League dhidi ya Jamhuri ya Czech, Ukraine na Uhispania mwezi huu wa Novemba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO