Pigo kuu kwa Raila Uhuru akishindwa kudhibiti Mlima Kenya

Pigo kuu kwa Raila Uhuru akishindwa kudhibiti Mlima Kenya

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kushindwa kudhibiti eneo la Mlima Kenya imezua tumbojoto katika kambi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Baada ya kuwatelekeza vinara wenzake wa muungano wa NASA; Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Musalia Mudavadi (Amani National Congress – ANC), Bw Odinga sasa ameweka matumaini yake yote kwa Rais Kenyatta kumsaidia kuingia ikulu 2022.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kushindwa kudhibiti siasa za eneo la Mlima Kenya ni pigo kwa Bw Odinga.Wakili Felix Otieno anasema kuwa Bw Odinga alitegemea Rais Kenyatta kupenya katika maeneo ya Mlima Kenya.

“Hatua ya Rais Kenyatta kushindwa kudhibiti eneo la Mlima Kenya kisiasa ni ishara kwamba Bw Odinga atakuwa na wakati mgumu kupenya eneo la Mlima Kenya iwapo atawania urais 2022,” anasema Bw Otieno.

Mgawanyiko katika eneo la Mlima Kenya umejitokeza zaidi baada ya Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata kuandika barua akimwelezea Rais Kenyatta kuwa wakazi wa eneo hilo hawataki Mpango wa Maridhiano (BBI).

Licha ya kushutumiwa vikali, Bw Kang’ata ameshikilia kuwa mambo yaliyokuwa ndani ya barua yake yanaonyesha hali halisi katika eneo la Mlima Kenya.Wakosoaji wa Bw Kang’ata wanasema kuwa huenda seneta huyo wa Murang’a anajiandaa kujiunga na mrengo wa Dkt Ruto kuwania ugavana 2022.

Japo Bw Odinga anakubaliwa na mabwanyenye kutoka Mlima Kenya, wengi wa wakazi wa tabaka la chini wanaonekana kuegemea mrengo wa Naibu wa Rais William Ruto.Mbali na kushindwa kudhibiti eneo la Mlima Kenya, Rais Kenyatta pia anaonekana kulemewa na jukumu zito la kuleta nidhamu ndani ya chama chake cha Jubilee.

Alhamisi, Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Emmanuel Wangwe pia alionyesha dalili za kutaka kumtoroka Rais Kenyatta, miezi michache baada ya kupewa wadhifa huo.

Bw Wangwe aliwataka viongozi wa jamii ya Waluhya kuungana na kumuunga mkono kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi ili kumpa nguvu za kufanya mazungumzo na Naibu wa Rais ili waamue mmoja kati yao atakayewania urais 2022.

Mbunge huyo wa Navakholo alipewa wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa baada ya Rais Kenyatta kumtimua mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

“Waluhya tumeshindwa kuungana na kuunga mkono Musalia Mudavadi ambaye tumemtawaza kuwa kiongozi wetu. Hakuna mtu mwingine ambaye amepewa wadhifa wa kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya isipokuwa wewe.

“Tunafaa kukuunga mkono ili tuwe imara, uketi na Naibu wa Rais ili mmoja wenu awe mwaniaji wa urais 2022,” akasema Bw Wangwe wakati wa ibada ya wafu ya kumuaga mama yake Bw Mudavadi aliyezikwa jana katika Kaunti ya Vihiga.

“Iwapo Rais Kenyatta hatabadili mbinu ili kuhakikisha kuwa anadhibiti eneo la Mlima Kenya kisiasa, Bw Odinga atakuwa na kibarua kigumu kupata kura 2022,” anasema Bw Otieno.

Viongozi wa ODM waliohojiwa na ukumbi huu walikiri kuwa mambo yatakuwa magumu kwa Bw Odinga endapo Rais Kenyatta hatarekebisha hali hiyo mapema.

You can share this post!

MTG United yaiadhibu Limuru Starlets 4-0

Uchaguzi mdogo wa useneta Machakos mtihani kwa umaarufu wa...