HabariSiasa

Pigo kuu kwa Ruto Pwani Kingi kuungana na Joho

August 16th, 2018 2 min read

KAZUNGU SAMUEL na AHMED MOHAMMED

GAVANA wa Kilifi Amason Kingi ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigia debe ziara za Naibu Rais William Ruto eneo la Pwani, Jumatano alikubaliana na mwenzake wa Mombasa Ali Hassan Joho kufanya kazi pamoja.

Hatua ya Bw Kingi inafasiriwa kuwa pigo kwa Bw Ruto, ambaye amekuwa akiungwa mkono na wabunge kadhaa wa chama cha ODM Pwani, chini ya uongozi wa gavana huyo.

Jumatano, Bw Kingi alisema kuwa kutakuwa na mikutano mingine kote Pwani, kwa lengo la kutimiza azma ya umoja wa Pwani.

“Hili sio jambo la siku moja na kukamilisha kila kitu. Ajenda sasa zimeanza na tutazunguka katika kila eneo. Najua itachukua muda lakini hatimaye tutaafikiana katika malengo yetu kama Wapwani. Sisi ni viongozi na nyuma yetu kuna watu ambao tunawaongoza,” akasema Bw Kingi.

Naye Joho alisema kuwa ari ya Pwani kutoa Rais wa taifa bado ingalipo, na kwamba muda umefika kwa viongozi wa eneo hilo kuangalia mbali kisiasa na kuacha tabia ya kuwapigia makofi viongozi wengine.

“Muda umefika ambapo sisi kama viongozi wa Pwani lazima tujiamini hadi katika uongozi wa kitaifa. Haiwezekani kwamba kila siku tutaendelea kuwa wafuasi wa watu wengine. Hata Pwani sasa tunaweza mara hii,” akasema Bw Joho.

Kauli ya wawili wao inafifisha kabisa matumaini ya Bw Ruto kuendelea kupigiwa debe Pwani, ikizingatiwa kuwa hata wabunge wawili waliokuwa mstari wa mbele wameamua kufyata ndimi zao.

Mbunge wa Malindi, Asha Jumwa na Suleiman Dori (Msambweni) ambao walikuwa wametangaza hadharani kuunga azma ya Bw Ruto kuwania urais mwaka 2022, wamenyamaza. Ingawa Bi Jumwa amekuwa mgonjwa, wadadisi wa siasa za Pwani wanaamini kuwa barua walizoandikiwa wawili hao na chama chao cha ODM pia huenda zimechangia kimya chao.

Chama hicho cha Chungwa kilikuwa kimewapa siku saba wawili hao waeleze kwa nini wasichukuliwe hatua, na hata kikasema kiko tayari kuweka wawaniaji wengine kwenye uchaguzi mdogo iwapo wanasiasa hao watajiuzulu.

Kwenye mkutano wa jana katika hoteli ya Flamingo eneo la Shanzu, magavana hao wa ODM walikutana na wawakilishi 175wa wadi kutoka kaunti zote sita za Pwani.

Mkutano huo ulijiri karibu wiki tatu baada ya Bw Kingi kukutana na wabunge 18 kati ya 21 wa Pwani, katika kilichoonekana kama mkakati wa kumpigia debe Bw Ruto.

Bw Joho alipongeza mwafaka kati ya Raila Odinga na Uhuru Kenyatta akisema umempatia nafasi yeye kama kiongozi katika Pwani kuwa na fursa nzuri ya kusukuma ajenda ya maendeleo kwa niaba ya wakazi wa Pwani.

“Mimi sasa hivi ninaweza nikaketi na Rais na kumwambia kwamba tunataka hili lifanyike katika bandari ya Mombasa na likafanyika. Huu ni mwanzo mpya ambao umekuja kwetu na lazima tuamue sasa, ” akasema.