Michezo

Pigo kwa AC Milan mkongwe Zlatan Ibrahimovic akipata jeraha

May 26th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

HUENDA taaluma ya usogora wa mshambuliaji mkongwe Zlatan Ibrahimovic imefikia mwisho baada ya kikosi cha AC Milan kufichua kwamba nyota huyo mzawa wa Uswidi amepata jeraha baya la mguu litakalomweka mkekani kwa kipindi kirefu.

Ibrahimovic, 39, aliumia vibaya mnamo Mei 25, 2020 alipokuwa akishiriki mazoezi kivyake uwanjani San Siro jijini Milan, Italia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na AC Milan, fowadi huyo wa zamani wa Ajax, Juventus na Inter Milan atatathminiwa zaidi na madaktari mnamo Mei 26 ili kubaini kiwango cha jeraha alilopata.

Hata hivyo, magazeti mengi nchini Italia yanashikilia kwamba mguu wa Ibrahimovic ulioumia ni ule uliowahi kumsumbua sana kati ya Januari na Februari baada ya jeraha baya alilowahi kupata akichezea Manchester United ya Uingereza mnamo 2016-2018 kurejea.

“Tutamkagua Jumanne ya Mei 26 na kutathmini ukubwa na ubaya wa jeraha lenyewe. Inahofiwa ni jeraha baya ambalo huenda ni tishio kubwa kwa taaluma yake ya soka katika siku zijazo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Milan.

Ibrahimovic alijiunga upya na Milan kwa mkataba wa miezi sita mnamo Disemba 2019 na anajivunia kuwafungia jumla ya mabao manne kutokana na mechi 10 za hadi kufikia sasa za Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Nyota huyo anajivunia kutandaza boli na kujitwalia mataji ya haiba katika soka ya Uhispania, Uinegreza, Italia na Ufaransa. Mbali na kuwahi kuwa mchezaji wa kikosi cha LA Galaxy nchini Amerika, amewahi pia kuwawajibikia Malmo, Barcelona na Paris Saint-Germain (PSG).

Aliwahi kuvalia jezi za Man-United chini ya ukufunzi wa Jose Mourinho na kuongoza miamba hao wa soka ya Uingereza kunyakua mataji ya Europa League na League Cup.