Pigo kwa afisa korti kuunga uamuzi wa gavana kumfuta

Pigo kwa afisa korti kuunga uamuzi wa gavana kumfuta

Na BRIAN OCHARO

MWANASIASA wa Chama cha ODM amepata pigo baada ya mahakama kukataa kufutilia mbali uamuzi wa Gavana Fahim Twaha kumtema kama mshauri wa kiuchumi wa serikali ya Kaunti ya Lamu.

Bw Shekue Kahale Kombo alikuwa amesimamishwa kazi Machi mwaka huu kwa madai ya kujihusisha na kampeni za mapema badala ya kutekeleza majukumu yake.

Hata hivyo, alielekea katika mahakama ya ajira na viwanda iliyo Mombasa akitaka uamuzi huo ubatilishwe kwa madai kuwa Bw Twaha hakufuata sheria wakati akimtimua.

Bw Kombo alitaka utekelezaji wa uamuzi huo wa gavana usitishwe na nafasi yake isipeanwe kwa mtu mwingine kwa madai kuwa hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kufutwa.

“Nilifutwa kazi ghafla wakati nilikuwa nikilipia mkopo niliochukuwa kutoka kwa benki,” alisema.

Hata hivyo Jaji Byram Ongaya alikataa kuruhusu ombi ilo akisema kuwa hakuna sababu ya msingi katika ombi hilo.Hii ni licha ya kuwa jaji alikubali katiba haikufuatiliwa wakati wa utekelezaji wa uamuzi huo.

“Licha ya kasoro za kiutaratibu kwa njia ambayo mwombaji alifutwa kazi, hajatoa sababu ya kupinga madai ya kuhusika katika kampeni za mapema,” alisema jaji huyo.

Mahakama ilisema kwa kukosa kubainisha suala kuhusu kampeni za mapema, ilionekana kuwa mlalamishi amekiri madai kuwa alihusika kwa kampeni hizo.

Bw Kombo aliteuliwa kuwa Mshauri wa Kiuchumi katika Serikali ya Kaunti ya Lamu, mnamo Aprili 2019, na mkataba huo unamalizika mwezi huo huo mwaka ujao.

Alikuwa amewania ubunge Lamu Mashariki 2017 kupitia ODM lakini hakushinda uchaguzini.

You can share this post!

Hamwezi kuzima hasla, Ruto aambia wapinzani

Jaji aliyetimuliwa adai alitemwa bila utaratibu