Pigo kwa Barcelona fowadi Lautaro Martinez wa Inter Milan akifichua malengo ya kusalia Serie A hadi atakapostaafu soka

Pigo kwa Barcelona fowadi Lautaro Martinez wa Inter Milan akifichua malengo ya kusalia Serie A hadi atakapostaafu soka

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Lautaro Martinez amesema kubwa zaidi katika matamanio yake ni kustaafu soka akivalia jezi za Inter Milan ambao kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Kwa mujibu wa Martinez ambaye ni raia wa Argentina, nia yake ni kurefusha mkataba wa sasa alio nao na Inter ili kuzima tetesi zozote kuhusu mustakabali wake kitaaluma, hatua ambayo itampa utulivu na wakati maridhawa wa kumakinikia majukumu yake kambini mwa waajiri wake.

Ungamo hilo la Martinez, 23, ni pigo kwa Barcelona waliokuwa na azma ya kumsajili fowadi huyo ili awe kizibo cha Lionel Messi anayetarajiwa kuondoka rasmi uwanjani Camp Nou mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Barcelona waliwahi kuweka wazi azma ya kumsajili Martinez mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 ila jaribio lao likagonga mwamba katika dakika za mwisho. Wakati huo, alitarajiwa kujaza nafasi ya fowadi Luis Suarez aliyejiunga na Atletico Madrid.

Katika mahojiano yake na gazeti la Gazzetta dello Sport nchini Italia, Martinez amesema kwamba ndoto ya kuchezea Barcelona sasa imezimika na azma yake ni kuongoza Inter kunyanyua idadi inayowezekana ya mataji.

Inter kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Serie A kwa alama 53, nne zaidi kuliko wapinzani wao wakuu AC Milan. Wanajivunia pengo la alama saba kati yao na mabingwa watetezi Juventus kadri wanavyolenga kutwaa taji la kwanza la Serie A baada ya miaka 11.

Kufikia sasa, Martinez amehusika pakubwa katika mafanikio ya Inter ikizingatiwa kwamba amefunga mabao 13 na kuchangia mengine sita kufikia sasa muhula huu.

Ushirikiano mkubwa kati yake na mshambuliaji wa zamani wa Everton na Manchester United umehisika zaidi huku Lukaku ambaye ni raia wa Ubelgiji akifunga magoli 17, moja pekee nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Juventus anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa Serie A kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Aston Villa wapepeta Leeds United na kuweka hai matumaini...

Visa vya uhalifu vyawatia hofu wakazi wa Thika