Habari Mseto

Pigo kwa familia korti kuikataza kuzika jamaa wake upya

June 15th, 2020 1 min read

NA DICKENS WASONGA

Mahakama Kuu ya Siaya Jumatatu imekataa kupeana amri kutolewa kwa mwili wa mgonjwa wa kwanza wa corona wa kaunti hiyo ili apewe heshima za mwisho na kuzikwa tena ilivyotakiwa na familia yake.

Familia ya James Oyugi Oyango, mfanyakazi wa zamani wa bandarini Mombasa ambaye mwili wake ulizikwa bila geneza katika kaburi fupi usiku wa manane na maafisa wa kaunti, ilienda kortini kuomba wapewe ruhusa kuufukua mwili huo ili wamzike tena upya katika mazishi yanayfuata utamanduni.

Jamaa hao walikua ni dadake Joan Akoth Ajuang na mwanawe Brian Oyugi, walioomba korti kufanya uchunguzi wa maiti ilikujua kilichosababisha kifo cha Bw Oyugi .

Waliomba korti ili kuwaruhusu watu 15 wa familia washuhudie mazishi ya pili yake katika maombi yaliyowasilishwa kortini Aprili 14.

Lakini jaji Roseline Aburili alisema kwamba hata kama korti ilipata kuwa kaunti ya Siaya ilikiuka amri za kuwazika waathiriwa wa corona, sheria zilizowekwa na shirika la afya duniani zinapinga kufukuliwa kwa mwili huo kwani kutaiweka familia na uma kwenye hatari zaidi.