Michezo

Pigo kwa Gabon na Arsenal baada ya jeraha la Aubameyang kuwa baya mazoezini

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amejiondoa katika kikosi cha Gabon kinachojiandaa kuvaana na Benin kirafiki mnamo Oktoba 11, 2020.

Hii ni baada ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kupata jeraha la kifundo cha mguu ambalo kwa sasa litamweka nje ya gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) litakalowakutanisha na Manchester City mnamo Oktoba 17, 2020 uwanjani Etihad.

Aubameyang ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Borussia Dortmund, alipata jeraha katika mchuano wa EPL uliokutanisha Arsenal na Sheffield United uwanjani Emirates mnamo Oktoba 4, 2020.

Sawa na vinara wa Shirikisho la Soka la Gabon, yalikuwa matarajio ya Aubameyang kwamba angalikuwa amepona kufikia Oktoba 11 ili aongoze timu yake ya taifa kupepetana na Benin jijini Lisbon, Ureno.

Kwa mujibu wa kocha Patrice Neveu wa Gabon, jeraha la Aubameyang lilianza kuwa baya akiwa kambini na akachochewa kumtema katika kikosi atakachokitegemea katika kibarua kijacho.

“Alirejea kambini mwa Arsenal na daktari wa kikosi hicho cha EPL akatuandikia kuhusu ukubwa wa kiwango cha jeraha linalouguzwa na Aubameyang,” akasema Neveu.

Jeraha hilo la Aubameyang ni pigo kubwa kwa kocha Mikel Arteta ambaye pia atakosa huduma za beki raia wa Scotland, Kieran Tierney, 23. Tierney kwa sasa anajitenga baada ya kuwa miongoni mwa wanasoka waliotangamana kwa karibu sana na mwanasoka Stuart Armstrong aliyepatikana na virusi vya corona kambini mwa timu ya taifa ya Scotland.