Michezo

Pigo kwa Klopp Mane kupatikana na corona

October 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI Sadio Mane wa Liverpool ameugua Covid-19 na kwa sasa amejitenga.

Habari za kuugua kwa mwanasoka huyo raia wa Senegal zinajiri siku tatu baada ya sajili mpya Thiago Alcantara kupatikana pia na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Liverpool, Mane alionyesha dalili za kuugua kwa kipindi kifupi kabla ya kuthibitisha kwamba ameanza kujihisi vizuri.

Mane, 28, alikuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilicholaza Arsenal 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 28, 2020. Mfumaji huyo hakupangwa katika kikosi kilichobanduliwa na Arsenal kupitia penalti katika EFL/Carabao Cup mnamo Oktoba 1.

“Sawa na hali iliyomtokea Alcantara, Liverpool wataendelea kuzingatia kanuni zote zilizopo za kukabiliana na Covid-19 na Mane atajitenga kwa muda unatakikana,” ikasema sehemu ya taarifa ya Liverpool.

Nyota huyo ambaye amefungia Liverpool jumla ya mabao matatu kufikia sasa, atakosa mechi ya EPL itakayowakutanisha waajiri wake na Aston Villa mnamo Oktoba 4 kabla ya EPL kuingia mapumzikoni.

Mechi ya kwanza ya Liverpool baada ya pumziko fupi litakalopisha mashindano ya kimataifa ni gozi la Merseyside litakalowakutanisha na Everton uwanjani Goodison Park mnamo Oktoba 17, 2020.

Mnamo Septemba 28, 2020, vinara wa EPL walifichua kwamba jumla ya watu 10 walikuwa wamepatikana na virusi vya corona katika matokeo ya hivi punde ya vipimo vya afya – hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwanzo wa msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO