Pigo kwa Leicester City jeraha la goti likiweka nje beki wao tegemeo hadi mwishoni mwa msimu huu

Pigo kwa Leicester City jeraha la goti likiweka nje beki wao tegemeo hadi mwishoni mwa msimu huu

Na MASHIRIKA

BEKI James Justin wa Leicester City sasa atakosa mechi zote zilizosalia katika kampeni za msimu huu baada ya kupata jeraha baya la goti.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 aliumia vibaya katika kipindi cha pili wakati wa mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA iliyowakutanisha na Brighton mnamo Februari 10, 2021.

Leicester wanaonolewa na kocha Brendan Rodgers waliibuka washindi wa mechi hiyo iliyochezewa ugani King Power kwa bao 1-0 lililofumwa kimiani na fowadi Kelechi Iheanacho mwishoni mwa kipindi cha pili.

Justin ambaye amechezea Leicester mechi 31 katika mashindano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu, aliondolewa uwanjani kwa machela baada ya kupata jeraha hilo.

Rodgers amesema kuumia kwa Justin ni pigo kubwa kwa kampeni za Leicester ambao ni miongoni mwa wagombezi halisi wa mataji matatu msimu huu – Kombe la FA, Europa League na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

“Ni mwanasoka aliyejaliwa uwezo wa kuwajibishwa katika nafasi yoyote kikosini. Yasikitisha sana kwamba sasa atasalia mkekani kwa kipindi kirefu,” akasema Rodgers ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Liverpool.

Kwa mujibu wa kocha huyo, Justin kwa sasa yuko katika hospitali moja jijini London na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti hapo kesho. Justin aliumia siku chache baada ya beki mwingine wa Leicester, Ricardo Pereira, kurejea uwanjani baada ya kuugua jeraha la goti kwa muda mrefu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Otieno ataka Zesco United ijitume zaidi Zambia

Jinsi ya kuandaa visheti