Michezo

Pigo kwa Liverpool Salah na Mane kupata majeraha

October 16th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

ZIMWI la jeraha linazidi kuwaandama wachezaji wanaokipigia kikosi cha kwanza cha timu ya Liverpool waliowajibikia mataifa yao katika michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Bara Afrika mwaka ujao wa 2019.

Mshambulizi matata Sadio Mane alipata jeraha kwa kuvunjika kidole chake cha gumba wakati timu yake ya taifa ya Senegal inapojiandaa kuonana kiume na Sudan katika mechi hizo za kufuzu  AFCON Jumanne Oktoba 2019.

Mwanadimba huyo wa zamani wa Southampton huenda akakosa mechi dhidi ya Sudan na anatarajiwa kurejea kambini mwa Liverpool baada ya mechi za kimataifa ili jeraha hilo litathminiwe upya kabla ya kupokezwa matibabu spesheli.

Liverpool pia walipata pigo la mwaka mshambulizi wao raia wa Misri Mohammed Salah alipoondolewa uwanjani wakati vijana wa ‘The Pharaohs’ walipowakalifisha Eswatini, timu ya taifa ya Swaziland 4-1 katika mojawapo ya mechi zizo hizo za kufuzu.

Majeraha haya ni pigo kwa mkufunzi wa Liverpool Jurgen Klopp ambaye awali alisikitikia majeraha mengi kikosi cheke hurejea nayo kila mara wanapotoka kuwajibikia majukumu ya kimataifa.

Jumamosi Oktoba 20 Liverpool watajibwaga uwanjani kwa mechi ya ugenini ya ligi kuu nchini Uingereza dhidi ya Huddersfield Town wakilenga kutoa ushindani mkubwa uongozini mwa msimamo wa jedwali la EPL.