Pigo kwa ‘mpango wa kando’ Uhuru akisaini sheria kuhusu urithi

Pigo kwa ‘mpango wa kando’ Uhuru akisaini sheria kuhusu urithi

Na CHARLES WASONGA

NI pigo kwa wapenzi wa pembeni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada unaowazima kudai mgao wa urithi wa mali ya marehemu wasiyeoana rasmi.

Wapenzi hao, maarufu kama mpango wa kando, na watoto wao, wamekuwa wakidai urithi wa mali ya wanaume waliofariki licha ya kwamba hawakuoana rasmi, kwa mujibu ya Sheria ya Ndoa.

Visa hivyo vimekuwa vikitokea baada ya vifo vya wanaume mashuhuri na matajiri.

Lakini kuanzia sasa, wanawake kama hao wataambulia pakavu baada ya Rais Kenyatta kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria ya urithi.

Kulingana na mswada huo uliodhaminiwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Opondo Kaluma, ni wanawake na wanaume walioko katika ndoa halali pekee, na watoto wao, watakaorithi mali ya marehemu.

“Mke au mume ambaye anapaswa kurithi mali, sharti awe kwenye ndoa inavyotambuliwa na Sheria ya Ndoa, sio rafiki au mpenzi jinsi ilivyo sasa,” akasema Bw Kaluma katika maelezo kuhusu mswada huo.

Kulingana na Mbunge huyo, ambaye ni wakili, nia yake katika kudhamini mswada huo ilikuwa kuzima mazoea ya watu kuchipuza kudai wagawiwe urithi wa mali ya marehemu kwa misingi kuwa walikuwa wapenzi na wakajaaliwa watoto.

“Kumekuwa na visa vingi ambapo watu, haswa wanaume, hufa na kisha watu ambao hawajahitimu kuwa wake wao, kulingana na Sheria ya Ndoa wanatokea wakati mke wako angali anaomboleza na kwenda kortini kudai sehemu ya mali yake,” Bw Kaluma akaeleza bungeni Agosti wakati wa mjadala kuhusu mswada huo.

Akaongeza: “Sio haki kwa mtu ambaye alikuwa akijificha asionekane na familia yake kudai mali ilhali sio mke wako kwa mujibu wa sheria. Hii ni sawa na kutapeli familia iliyofiwa.”

Kwa mfano, siku chache baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Matungu, Justus Murunga Novemba 2020, mwanamke kwa jina Agnes Wangui aliwasilisha kesi mahakamani akidai wanawe wawili waorodheshwe kama warithi wa mali ya marehemu.

Mwanamke huyo alitaka mazishi ya mbunge huyo yasimamishwe kwa muda, hadi matakwa yake yashughulikiwe.

You can share this post!

Serikali ya wakaidi wa sheria

Tusker, Gor zaruhusiwa kutumia uga wa Nyayo

T L