Habari MsetoSiasa

Pigo kwa Mudavadi hatua ya kutimua Malala ikigonga ukuta

July 8th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi alipata pigo jingine Jumanne wakati hatua ya chama chake kumtimua Seneta wa Kakamega Cleophas ilipokataliwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu.

Mwaka uliopita, jaribio la ANC kumfurusha Mbunge Maalum Godfrey Osotsi kwa madai ya kuasi uongozi wa chama hicho liligonga mwamba wakati Bunge la Kitaifa lilipokataa kuidhinisha hatua hiyo.

Jana, Bi Nderitu alimwandikia Katibu Mkuu wa ANC, Bw Barack Muluka, akisema kufurushwa kwa Seneta Malala hakukufuata taratibu zifaazo za kisheria na katiba ya chama hicho.

“Baada ya kuchambua ombi la kumrufusha mwanachama aliyetajwa, afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa imetambua kuwa taratibu za kumwadhibu hazikukamilishwa kwa muda uliowekwa kulingana na Katiba ya ANC,” akasema.

“Vile vile, Baraza la Uongozi (NGC) halikuidhinisha wanachama wapya wa kamati ya nidhamu, walioteuliwa na Baraza Kuu (NEC), kulingana na Katiba ya ANC,” akaongeza Bi Nderitu.

Mwezi uliopita, mkutano maalum wa NGC ulioongozwa na Bw Mudavadi uliamua kwa kauli moja kumfurusha Seneta Malala kwa kuegemea chama cha ODM na kutoheshimu uongozi wa chama hicho.

Bw Malala anatuhumiwa kukiuka katiba ya chama hicho na sheria ya vyama vya kisiasa kwa kumpigia debe mgombeaji wa ODM Imran Okoth ilhali ANC ilidhamini Bw Eliud Owalo katika uchaguzi huo.

ANC ilijitetea kuwa ilifuata sheria na taratibu zifaazo kwa kumwamuru Seneta Malala afike mbele ya Kamati yake ya Nidhamu ili ajitetee dhidi ya madai hayo lakini akakataa.

Lakini Bw Malala alisisitiza hawezi kuomba msamaha kwa ANC na yuko tayari kurejea debeni kutetea kiti chake kwa chama kingine uchaguzi mdogo ukiitishwa.

Bw Malala alisema hawezi kuvunja uhusiano wake na ODM pamoja na kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga.

“Narudia kusema kuwa nitaendelea kujihusisha na chama chama ODM ambacho kina sura ya kitaifa.Nashikilia kuwa siwezi kuhudhuria kamati ya nidhamu ambayo ni haramu,” akasema