Pigo kwa Obado korti ikikataa kesi dhidi yake kusikilizwa Migori

Pigo kwa Obado korti ikikataa kesi dhidi yake kusikilizwa Migori

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Kisumu imekataa kuhamisha kesi ya ufisadi inayomkabili Gavana wa Kaunti ya Migori Okoth Obado na watoto wake wanne kusikilizwa katika mahakama ya Migori.

Jaji Fred Ochieng alitupilia mbali ombi lililowasilishwa na mshukiwa mkuu katika kashfa hiyo ya Sh2.5 bilioni Bw Jared Peter Odoyo Kwaga kesi hiyo ihamishwe kutoka mahakama ya Nairobi hadi Migori.

Katika ombi lake Bw Kwaga alisema washukiwa wengi katika kesi hiyo ni wakazi wa Migori na hugharamika kiasi kikubwa cha pesa kusafiri hadi Nairobi na kukodisha makazi.

Bw Obado ameshtakiwa kwa kupotea kwa zaidi ya Sh256 milioni.

Bw Kwaga alikuwa amemweleza Jaji Ochieng makosa yalifanyika Migori na kesi haifai kusikilizwa Nairobi.

Lakini Jaji Ochieng alitupilia mbali ombi hilo akisema Bw Kwaga angeliwasilisha katika mahakama ya Milimani aliposhtakiwa siku ya kwanza.

Jaji Ochieng aliendelea kusema mshtakiwa hastahili kuchagua mahakama itakayosikiliza kesi inayomkabili.

“Itakuwa ukiukaji wa maadili kumruhusu mshukiwa kuwasilisha ombi Kisumu ilhali kesi inasikilizwa Nairobi akiomba kesi ihamishwe hadi Migori au mahakama iliyoko karibu,” Jaji Ochieng alisema.

Kesi hiyo ya ufisadi inahusisha familia ya Bw Obado na ile ya Bw Kwaga.

Familia hizi zinashtakiwa kwa kushiriki ufisadi uliopelekea kaunti ya Migori kupoteza zaidi ya Sh2.5 bilioni kati ya 2013 na 2017 katika kipindi cha kwanza cha Gavana Obado.

Katika mashtaka 27, Bw Obado na watoto wake wanakabiliwa na mashtaka 22.

Baadhi ya akaunti za Bw Obado na mali zake zimetwaliwa na Serikali.

Jaji huyo alisema uhalisi wa pale kesi imepelekwa sio jukumu la washtakiwa na mawakili wao.

Washtakiwa waliomba hakimu mkuu Lawrence Mugambi anayesikiliza kesi hiyo aitengee siku ya mbali kuwezesha mabinti wawili wa Bw Obado walioshtakiwa pamoja naye kujifungua.

  • Tags

You can share this post!

Malalamiko ya Nigeria yasababisha mashindano ya handiboli...

Uhuru mbioni kuwapatanisha Raila, Museveni

T L