Pigo kwa OKA Kanu ikisema haitaacha kuunga Jubilee

Pigo kwa OKA Kanu ikisema haitaacha kuunga Jubilee

Na JUSTUS OCHIENG

Mipango wa kuhalalisha muungano One Kenya Alliance (OKA) ulipata pigo baada ya chama cha Kanu kusema hakina mipango ya kukatiza ushirikiano wake na chama tawala cha Jubilee.

Vinara wa OKA ni Musalia Mudavadi (Amani National Congress), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Kulingana na sheria, hakuna chama kinachoweza kuwa katika miungano miwili kwa wakati mmoja.

Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Wetang’ula wamesema kwamba watajiondoa katika muungano wa NASA waliosema ni sehemu ya historia yao.

“Kilichobaki sasa ni hawamu ya mwisho ya kuzika muungano huo ambayo ni kufuatilia matumizi ya pesa,” walisema.

Lakini katibu mwenyekiti wa Kanu,Nick Salat jana alisema kwamba muungano wa chama hicho na Jubilee uliidhinishwa na Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) na ni wao wanaofaa kupitisha kijionndoe.

Bw Salat alisema hayo siku moja baada ya OKA ambao Kanu ni mwanachama kutangaza kwamba chama hicho cha uhuru ni lazima kijiondoe katika muungano wake na Jubilee kabla ya kujiunga rasmi na muungano huo mpya.

“Hauwezi kuwa mwanachama wa miungano miwili kwa wakati mmoja chini ya sheria. Lazima hii ieleweke. Kwa hivyo, Kanu itaacha Jubilee na itatangazwa rasmi,” alisema naibu mwenyekiti wa Wiper

Mutula Kilonzo Jnr aliyesoma taarifa kwa niaba ya vinara wa OKA.

Aliongeza: “Tukiunda One Kenya Alliance, vinara wa vyama vyote vitatu lazima wataondoka Nasa na lazima Kanu iache Jubilee. Kila muungano, ukiwemo wa Jubilee utaisha uchaguzi mkuu ujao.”

Bw Moi alisema kwamba ilikuwa mapema kujadili hatua ya Kanu kujiondoa katika muungano wake na Jubilee.

“Swali hilo halifai kwa wakati hu lakini kuna mazungumzo yanayoendelea,” akasema Bw Moi.

Lakini jana, Bw Salat aliambia Taifa Leo kwamba muungano wa Kanu na Jubilee unadumu hadi mwisho wa muhula wa bunge la sasa na hawana sababu ya kuvunja mapema.

“Kwa sasa, sote tunajipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2022 na hatufai kufikirika vingine. Fauka ya hayo, mkataba wetu na Jubilee unaendelea hadi 2022 na tunaweza kushiriki muungano mwingine ikibidi kufanya hivyo,” alisema.

Alisema kwamba Kanu haiko tayari kuacha kushirikiana na serkali.

You can share this post!

Eid: Viongozi wavunja desturi ya Kiislamu sababu ya siasa

Raila abaki jangwani