Pigo kwa Ruto Jubilee ikifufuka Mlima Kenya

Pigo kwa Ruto Jubilee ikifufuka Mlima Kenya

GITONGA MARETE Na ALEX NJERU

VUGUVUGU la Azimio la Umoja linaloongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga limeanza kupata uungwaji mkono katika kaunti za Mlima Kenya Mashariki.

Hii ni baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto kuanza kukabiliwa na upinzani mkali katika maeneo hayo ambako awali, chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilishabikiwa kwa wingi.

Kaunti za Embu, Tharaka Nithi na Meru sasa zimeanza kukumbatia ‘injili’ ya Azimio la Umoja baada ya kucheza densi ya Dkt Ruto kwa miaka minne iliyopita.

Mojawapo ya sababu za mabadiliko haya ni kuzinduliwa upya kwa chama cha Jubilee katika eneo hilo.

Aidha, hatua ya viongozi wakuu wa Mlima Kenya Mashariki wakiwemo Gavana Kiraitu Murungi (Meru), Waziri wa Kilimo Peter Munya na mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore kuunga mkono Bw Odinga ni sababu nyingine.

Akiendesha kampeni katika eneobunge la Igembe Kaskazini Ijumaa iliyopita, seneta wa Meru Mithika Linturi ambaye amejitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana kwa tiketi ya UDA alikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vijana waliokuwa wakiimba nyimbo za kusifu Azimio la Umoja.

Hata hivyo, Bw Linturi alipuuzilia mbali kisa hicho na kuwashutumu wapinzani akidai kuwa walikodi vijana hao kumzoma.

Wafuasi wa Waziri Munya wamesema watamuunga mkono Gavana Murungi katika kampeni zake za kuvumisha Bw Odinga katika eneo hilo.

Wafuasi wa Bw Munya ambao wamekuwa wanachama wa chama cha PNU wamekuwa wakijiunga na Jubilee kwa wingi.

Wanasema wako tayari kupambana na wapinzani wao kutoka chama cha UDA.

Katika kaunti za Tharaka Nithi na Meru, wafuasi wa Bw Munya wameamua kuwania viti mbalimbali kwa kutumia Jubilee, ambayo ni maarufu kuliko PNU.

Aliyekuwa mbunge wa Tigania Magharibi David Karithi ambaye alikuwa mwanachama wa PNU sasa anawania kumuondoa mbunge wa sasa Dkt John Mutunga anayetetea kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Naye aliyekuwa mshauri katika Wizara ya Kilimo, Julius Kimathi, atakabiliana na mbunge wa Imenti ya Kati Kirima Ngucine wa chama cha UDA.

Atawania kwa tiketi ya chama cha Jubilee, sawa na Bw Karithi.

Katika kaunti ya Kirinyaga, aliyekuwa Seneta Daniel Karaba aligura chama cha The Service Party (TSP) chake Mwangi Kiunjuri na kujiunga na Jubilee.

Alipokewa na Katibu katika Wizara ya Usalama Karanja Kibicho.

Wakati wa uzinduzi wa kampeni za wawaniaji wa Jubilee katika eneobunge la Imenti Kusini Ijumaa wiki jana, naibu kiongozi wa Jubilee Kinoti Gatobu alisema Azimio la Umoja wanapenya eneo hilo kwa kasi mno.

Bw Gatobu alishuhudia kuidhinishwa kwa Dkt Shadrack Mwiti kuwa mgombeaji wa Jubilee katika eneobunge la Imenti Kusini.

You can share this post!

MUME KIGONGO: Kunenepa matiti ni kawaida lakini kunaweza...

Karamu ya mbuzi yaokoa mshukiwa wa mauaji

T L