Pigo kwa Serikali korti ikiruhusu Miguna kurejea

Pigo kwa Serikali korti ikiruhusu Miguna kurejea

Na RICHARD MUNGUTI

SERIKALI imepata pigo tena baada Mahakama ya Rufaa kuruhusu mwanaharakati, na wakili mbishi, Dkt Miguna Miguna aliyefurushwa chini baada ya kumwapisha kinara wa ODM Raila Odinga kurejea nchini kutoka Canada anakoishi.

Mnamo Juni 4, majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Roselyn Nambuye, Wanjiru Karanja na Mohammed Warsame walitupilia mbali ombi la Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki kubatilisha uamuzi wa Jaji Enock Mwita wa kuharamisha kufurushwa kutoka nchini kwa Dkt Miguna Februari 2018.

Majaji Nambuye, Karanja na Warsame walisema Serikali ilishindwa kuthibitisha haikukandamiza haki za Dkt Miguna ilipofutilia mbali paspoti yake na kufuta uraia wake ilhali ni raia wa Kenya aliyezaliwa eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu mwaka wa 1962.

Majaji hao walisema serikali ilishindwa kuthibitisha jinsi ‘ilivyoathiriwa na uamuzi wa Jaji Mwita kwamba iliharibu nyumba ya Miguna Feburuari 2, 2018 alipokamatwa na maafisa wa polisi na kuzuiliwa katika vituo kadhaa vya polisi’.

‘Serikali kupitia kwa Waziri wa Usalama na Masuala ya Kigeni imeshindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha jinsi agizokuwa Miguna akubaliwe kurudi nchini na alipwe fidia ya Sh7.2 milioni litakavyoiathiri,’ majaji Nambuye, Karanja na Warsame walisema katika uamuzi wao.

Mwanasheria mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Alexander Muteshi, walisema endapo agizo la mahakama kuu halitasitishwa, huenda maafisa sita wakuu serikalini akiwemo Dkt Matiang’i wakashtakiwa kwa kudharau na kukaidi maagizo ya mahakama.

Dkt Matiang’i, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji, Meja mstaafu Gedion Kihalangwa, aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet, Mkurugenzi wa DCI George Kinoti, Afisa Msimamizi wa Polisi wa uwanja wa ndege wa JKIA, Afisa aliyesimamia kikosi cha Flying Squad na mwanasheria mkuu (AG) walishtakiwa kwa kukandamiza haki za Miguna.

Ni maafisa hawa sita wakuu serikalini waliowasilisha masuala 14 ya kuamuliwa katika rufaa waliyowasilisha mbele ya majaji hao watatu wa mahakama ya rufaa.

‘Tunaomba mahakama ibatilishe maagizo kwamba tulikandamiza haki za Miguna.

Alipwe fidia ya Sh7.2 milioni, apewe pasipoti, arudi nchini na atambuliwe kuwa raia wa Kenya,’ Mwanasheria Mkuu alirai Mahakama ya Rufaa Vile vile, Jaji Mwita alisema kufurushwa kwa Dkt Miguna kutoka nchini hadi Canada baada ya Polisi kuagizwa imfikishe katika mahakama kuu ni ukaidi wa hali ya juu na ukiukaji wa haki za kimsingi za mwanasiasa huyo.

Kufuatia vitendo hivyo, Jaji Mwita aliamuru Serikali imlipe Dkt Miguna fidia ya Sh7. 2 milioni kwa kukandamiza haki zake.

Pia Jaji Mwita aliamuru Dkt Miguna alipwe Sh270, 000 kwa kuharibiwa kwa makazi yake katika mtaa wa kifahari wa Runda, Nairobi.

Baada ya kufurushwa kutoka Kenya shirika la kutetea haki za binadamu nchini (KNHRC) and chama cha wanasheria nchini (LSK) ziliwashtaki maafisa wakuu serikali na kuomba idara ya uhamiaji impe Miguna pasipoti nyingine na kumruhusu arudi nchini kwa vile ni raia wa Kenya.

Katika kesi hiyo LSK na KNHRC waliomba mahakama iamue ikiwa Mkenya anaweza kupoteza uraia wake kwa kupata uraia wa nchi nyingine.

Katika uamuzi wao majaji watatu walisema hili ni suala nyeti ambalo lapasa kuamuliwa katika kesi aliyowasilisha mwanasheria mkuu.

You can share this post!

Demu afumaniwa akiroga wakwe

Kufa ghafla kwa TB Joshua kwawashtua wafuasi wake