Habari Mseto

Pigo kwa ushairi mlumbi maarufu Shamte akifariki

February 10th, 2020 2 min read

MISHI GONGO na HASSAN MUCHAI

ULIMWENGU wa ushairi unaomboleza kifo cha mshairi mkongwe Abdallah Ali Shamte (pichani kushoto), aliyejulikana kwa lakabu “Mtumwa wa Mungu.”

Alifariki Jumapili usiku nyumbani kwake mjini Mombasa.

Mzee Shamte amekuwa akiugua kwa muda hali iliyomzuia kutembea kwa mwendo mrefu.

Marehemu aliswaliwa katika msikiti wa Kwa-Shibu na kuzikwa maziara ya Sargoi jana mchana.

Kifo chake kimeongeza idadi ya washairi wakongwe walioaga, ambao ni pamoja na Hassan Mwalim Mbega, Sheikh Ahmed Nabhany, Musa Mzenga, Abdallah Chombo, na Said Kizere miongoni mwa wengine.

Marehemu Shamte alizaliwa 1948 katika mtaa wa Mwembe Kuku Mjini Mombasa. Alianza masomo yake ya msingi katika shule ya Arab School ambayo sasa inafahamika kama Serani.

Baadaye alijiunga na Arab Secondary School kabla ya kusajiliwa na Taasisi ya Kiswahili ya Lumumba mjini Dar es salaam, Tanzania.

“Mtumwa wa Mungu’’ kama anavyojulikana kishairi, alikuwa mshairi wa kuumbuana na wakati mwingine mtoaji nasaha.

Alipotaka kumnyamazisha adui, alikuwa akitumia majina makubwa ya kujigamba kwa kujiita “Mshairi bora’’ na alipotaka kutoa nasaha alikuwa akijiita “Mtumwa wa Mungu”.

Tajriba yake ya utunzi akiwa mtoto mdogo imemfanya kuvuma kote Afrika Mashariki.

Kuna wakati mashairi yake yalikuwa yakitawala idhaa ya redio Voice of Kenya na kisha KBC kupitia kipindi cha mashairi kilichokuwa kikisimamiwa na Khadija Ali.

Ilikuwa muhali sana kukosa tungo zake zikighaniwa na Abdallah Mwasimba.

Shairi lake la kwanza alilitunga mwaka 1965 kujiliwaza baada ya kukimbiwa na mpenzi wake:

Amenihama nyumbani, wala sijui sababu,

Nikamlilie nani, sumbuko lilonisibu,

Sumbuko lilonisibu, wallahi lanikodesha,

Roho yangu matilibu, hali kunifurahisha,

Muhibu kunighilibu, sipendi yangu Maisha.

Kwa miaka 54, Bw Shamte alichangia mashairi katika magazeti. Kutokana na kifo cha mshairi huyo Mkuu wa Taifa Leo/Jumapili, Bw Peter Ngare alisema ni pigo kwa gazeti hili.

“Taifa Leo tumepata pigo kubwa. Itachukua muda kuziba pengo la Shamte katika kumbi za mashairi. Alikuwa mshairi na mlumbi shupavu wa miaka mingi,” akasema.

Wengine waliotuma risala zao ni Juma Ali Shumbana, Rajab Pilau, Wilson Ndung’u, Juma Salim Makayamba, Cornelius Mutisya, Hassan Morowa, Ismail Bakari, Kinyua King’ori na Abdul Noor.