Habari Mseto

Pigo kwa Viusasa na Skiza Tunes serikali ikibadilisha mfumo

January 15th, 2020 1 min read

Na PETER MBURU

WATOAJI huduma za burudani na muziki mitandaoni na kwenye simu kama vile Viusasa na Skiza, ama hata vyombo vya habari hawataruhusiwa kupokea malipo ya huduma hizo kwa niaba ya wasanii tena.

Badala yake, pesa hizo zitakuwa zikielekezwa katika akaunti itakayosimamiwa na serikali ili wasanii husika walipwe ipasavyo.

Amri hiyo ilitolewa na Rais Uhuru Kenyatta jana, ambapo alisema mitandao hiyo haijakuwa ikiwalipa wasanii vyema kulingana na vipaji vyao vya usanii.

Rais Kenyatta alisema japo wasanii wana uwezo wa kuzalisha Sh2 bilioni kila mwaka kupitia kazi hizo, ni Sh200 milioni pekee ambazo zimekuwa zikikusanywa na mitandao hiyo, na vyombo vingine vya habari vinavyoendesha huduma sawia.

Alisema maelewano yalifikiwamnamo Desemba 20 mwaka uliopita kuwa, ukusanyaji wa pesa za kazi za wasanii uwe ukisimamiwa na shirika la kiserikali, ambalo litakuwa likiwalipa baada ya muda fulani.

“Mfumo wa sasa ambapo wasanii wanashirikiana na mifumo ya kidijitali kama Skiza na Viusasa utavunjwa. Wasanii wote watahitajika kujisajili na Idara ya Usajili wa wamiliki wa mali bunifu, ili wawe wakilipwa pesa zao,” Rais Kenyatta akasema.