Pigo kwa waandalizi wa Michezo ya Shule baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku shughuli zote zisizo za kiakademia shuleni kwa siku 90

Pigo kwa waandalizi wa Michezo ya Shule baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku shughuli zote zisizo za kiakademia shuleni kwa siku 90

Na BRIAN YONGA

WAANDALIZI wa michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari humu nchini wamepata pigo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku shughuli zote zisizo za kiakademia kwa siku 90.

Katika agizo lililotolewa na Rais mnamo Jumapili, masuala yote ya michezo, drama, muziki, kutolewa kwa tuzo na ziara za wanafunzi na walimu miongoni mwa shule ni hayataruhusiwa kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Habari hizo ni za kusikitisha sana kwa vinara wa Chama cha Michezo ya Shule za Upili (KSSSA) na Chama cha Michezo ya Shule za Msingi (KPSSA) ambavyo vina idhini ya kuandaa michezo miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na upili humu nchini.

Awali, Peter Orero ambaye ni Mwenyekiti wa KSSSA alikuwa amefichua mipango ya kuandaa kikao na Wizara ya Elimu ili kujadili kuhusu jinsi ya kurejelewa kwa shughuli za michezo miongoni mwa wanafunzi shuleni.

“Wanafunzi wote hawana uwezo unaolingana katika masuala ya masomo ya vitabuni. Kunao wanaojivunia talanta na vipaji mbalimbali na michezo ambayo tumekuwa tukiandaa kwa kipindi kirefu kilichopita kimedhihirisha hilo,” akatanguliza Orero.

“Hivyo, itakuwa vyema zaidi iwapo Serikali itaturuhusu kurejelea shughuli za michezo na mashindano mbalimbali shuleni,” akasema Orero ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Dagoretti.

KSSSA tayari imeandaa semina katika takriban sehemu zote za humu nchini ili kuhamasisha walimu kuhusu jinsi ya kufanikisha shughuli za michezo mbalimbali chini ya uzingativu wa kanuni zilizopo za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Kutolewa kwa idhini ya kurejelewa kwa baadhi ya michezo humu nchini mwishoni mwa 2020 kulikuwa kumewapa maafisa wa KSSSA na KPSSA matumaini ya mkondo huo kufuatwa mwaka huu baada ya shule kufunguliwa.

Mnamo 2020, vyama hivyo vya michezo havikuweza kuandaa baadhi ya mashindano yao baada ya shule kufungwa ghafla mwanzoni mwa mwezi Machi kutokana na janga la corona.

KSSSA ilikuwa imeratibu shughuli nyingi za michezo mwaka huu wa 2021 ambapo kilele chake kingekuwa ni Kenya kuwakilishwa kwenye Michezo ya Shule Duniani jijini Jinjiang, China kwa mara ya kwanza katika historia.

Fainali za Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Upili katika eneo la Afrika Mashariki zilikuwa pia ziandaliwe Kenya kwa mara ya kwanza mwaka huu baada ya miaka minne.

Kisa cha kwanza cha maambukizi ya corona kiliporipotiwa humu nchini mnamo Machi 12, Michezo ya Muhula wa Kwanza miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili ilikuwa imefikia kiwango cha kaunti huku washindi wakiwa na matarajio ya kufuzu kwa hatua ya kitaifa.

Miongoni mwa michezo ambayo huandaliwa katika Muhula wa Kwanza ni vikapu, raga kwa wachezaji saba na 15 kila upande, hoki, uogeleaji, handiboli na riadha.

Zaidi ya wanafunzi 1,900 walitarajiwa kukongamana katika Shule ya Upili ya Kapsabet Boys na Shule ya Upili ya Kapsabet Girls kwa fainali za michezo ya kitaifa ya Muhula wa Kwanza miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili kati ya Aprili 4-11, 2020.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kajiado All Stars wapepeta Kayole Youth na kutinga...

AC Milan wachabanga Benevento na kudhibiti tena kilele cha...