Habari

Pigo kwa Wabukusu tohara ikiahirishwa

June 20th, 2020 2 min read

Na BRIAN OJAMAA

UTAKUWA mwaka wa kusahau kwa wakazi wa magharibi hasa jamii-ndogo ya Wabukusu kwani utamaduni wanaouthamini sana wa tohara ya wavulana maarufu kama Sikhebo utakosekana mwaka huu.

Desturi ya upashaji tohara ambayo huja kila baada ya miaka miwili haitatekelezwa mwaka huu kutokana na janga la corona ambalo huenea kwa kasi kutokana na mikusanyiko ya watu.

Sikhebo huja kila mwezi wa Agosti mwaka wa pili mbele. Huwa ni msimu wa sherehe na furaha kwa janibu za Mulembe na husubiriwa kwa hamu na ghamu kubwa.

Wavulana wanaobalehe huwa wamejiandaa kisaikolojia kukabiliana na harakati ngumu ya kupashwa tohara hiyo ambayo huanza kwa kutembezwa makazini na barabarani kwa nyimbo za kitamaduni (khuminya) kwa siku kadhaa kabla ya kuishia kwa kupakwa tope alfajiri (khubalikha) na hatimaye mhusika kukabiliana na kisu kikali cha ngariba (khukheba).

Baada ya kubaini kuwa huenda kufikia mwezi Agosti ugonjwa huo hautakuwa umeisha, wazee wa jamii ya Waluhyia walilazimika kuchukua hatua hiyo.

Serikali imepiga marufuku mikusanyiko yoyote ya watu wengi ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Wakiwahutubia wanahabari mjini Bungoma jana, wazee hao kutoka jamii za Wabukusu, Watachoni, Wabaatura na Wasabaot walisema kuwa mwaka huu umejaa mikosi.

Wakiongozwa na Mzee Richard Walukano, kutoka Baraza la Wazee la Wabukusu, wazee walisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa kutokana na tishio la virusi hivyo, ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu kote duniani. Walisema kuwa uamuzi huo si wa kwanza, kwani ushafanywa tena katika siku za nyuma.

“Hii si mara ya kwanza kwetu kuchukua hatua kama hii. Tulifanya uamuzi kama huo katika miaka ya thelathini, baada ya ugonjwa hatari kuzuka nchini na katika miaka ya sitini wakati vita vilikuwa vikiendelea katika sehemu kadhaa hapa nchini,” akasema.

Alieleza kuwa ikiwa kuna yeyote atakiuka agizo hilo la wazee, basi kuna hatari ya mwanawe kukumbwa na mkosi ama laana.

Mzee Wekesa Wasilwa, kutoka Baraza la Wazee la Watachoni, alisema kuwa ingawa huenda hatua hiyo ikavuruga mpangilio wa zoezi hilo katika siki zijazo, hawakuwa na lingine ila kuiahirisha.

Mwenyekiti wa ngariba katika Kaunti ya Bungoma, Bw Sinimo wa Omukolongolo, alisema kuwa kuna shughuli nyingi ambazo huandama hafla hiyo, hivyo kuiandaa kungewaweka wenyeji kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

“Huwa tuna shughuli nyingi za wakazi kutangamana kama unywaji pombe ya kienyeji, uimbaji wa nyimbo na uchezaji densi. Hayo yote yamepigwa marufuku na Wizara ya Afya,” akasema.

Aliwaomba wazazi wanaotaka wanao kutahiriwa kungoja hadi hali ya kawaida itakaporejea.

“Wazee wetu watamchinja mbuzi na kuangalia maini yake ili kutupa utabiri wa hali itakavyokuwa katika kipindi kilichobaki mwaka huu,” akasema.

Sinino alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote ambaye atakiuka agizon lililotolewa.

Alisema kuwa vijana watakaotahiriwa baada ya hali ya kawaida kurejea watapewa jina maalum la kiukoo.

Hafla ya mwisho ya upashaji tohara ilifanyika mnamo 2018.

Vijana hupewa majina ya kiukoo baada ya kila hafla.

Upashaji tohara wa Wabukusu ni miongoni mwa hafla za kitamaduni zinazofuatiliwa sana, kwani huwavutia zaidi ya watalii 40,000 wa kigeni na hapa nchini.

Wakati wa hafla hiyo, anayetahiriwa huenda kwa mjombake, ambako hafla maalum huandaliwa huku pia fahali akichinjwa.

Huwa anapewa baadhi ya nyama kupeleka nyumbani kwao.

Siku inayofuata, huwa anapelekwa mtoni nyakati za alfajiri ambapo mwili wake wote huwa unapakwa matope. Anaporejea, huwa anapashwa tohara katika lango kuu la kuingia kwao akiwa ameangalia upande wa Magharibi.