Habari

Pigo kwa Waiguru MCAs wakikataa kuidhinisha bajeti

July 16th, 2020 2 min read

Na GEORGE MUNENE

GAVANA wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, alipata pigo Jumatano, baada ya madiwani anaozozana nao kukataa kuidhinisha bajeti ya serikali yake.

Madiwani hao walikataa taarifa ya Bi Waiguru kuhusu bajeti ya mwaka wa 2020/2021 na kuitupilia mbali. Katika mswada uliowasilishwa na diwani wa wadi ya Baragwi, Bw David Mathenge, madiwani 25 walipiga kura kukataa bajeti hiyo. Sita hawakuhudhuria kikao cha Jumatano.

Diwani mmoja alikataa kupiga kura na mmoja akaunga bajeti ya Gavana Waiguru huku mzozo wa kisiasa kati yake na madiwani hao, unaotishia kulemaza huduma katika kaunti hiyo, ukiendelea kuchacha.

Madiwani hao walisisitiza kwamba bajeti iliyowasilishwa na gavana haikuwa ya kuwafaidi wakazi na kwa hivyo hawakuwa na budi kuikataa.

“Tumetambua kwa masikitiko kwamba serikali ya Kaunti ilitenga Sh30 milioni za basari kwa wanafunzi maskini badala ya Sh140milioni tulizokuwa tumependekeza. Pesa za maendeleo katika wadi pia zimepunguzwa. Serikali hii haijali maslahi ya wakazi wa kawaida na hatuwezi kupitisha bajeti kama hiyo,” Bw Mathenge alisema.

Diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kaunti kuhusu bajeti, aliwahimiza wenzake kumzima gavana akimlaumu kwa kupuuza ushauri wa bunge la kaunti.

Naye kiongozi wa wengi, Bw Kamau Murango, alimlaumu Bi Waiguru kwa kupuuza idara ya mazingira na jinsia kwa kukosa kuitengea pesa za kutosha.

“Bajeti hii haiwezi kukubalika na inafaa kukataliwa kabisa,” alisema Bw Murango.

Bi Waiguru alikuwa amekataa kutia sahihi bajeti madiwani walipoifanyia mabadiliko na akairudisha katika bunge la kaunti na taarifa akiwaeleza makosa waliyofanya madiwani.

Aliwaeleza kuwa aliwasilisha bajeti ya mwaka wa 2020/2021 katika bunge la kaunti iidhinishwe lakini madiwani walimrudishia bajeti mpya. Alisema madiwani walibadilisha asilimia 30 ya bajeti ya serikali yake kinyume na sheria ya pesa za umma ya 2015 inayosema bunge la kaunti linafaa kubadilisha asilimia moja.

Bi Waiguru alisema mbali na hatua ya madiwani kuwa kinyume na sheria, hangekubali mabadiliko waliyofanyia bajeti ya serikali yake.

Aliwalaumu madiwani hao kwa kuondoa Sh300 milioni zilizotengewa mishahara ya wahudumu wa afya na kuzihamishia ujenzi wa afisi za madiwani katika wadi zao.

“Hii haikubaliki kabisa ikizingatiwa kuwa wahudumu wa afya wanahatarisha maisha yao wakipigana na janga la corona na itaweka maisha ya wakazi hatarini kwa kukosa kupata huduma za matibabu,” alisema.

Aliongeza kuwa madiwani waliondoa Sh20 milioni zilizotengewa mishahara ya vibarua ambao husafisha mazingira na vituo vya afya hasa wakati huu wa janga la corona. Madiwani hao pia waliondoa Sh14.6 milioni za mafuta ya ambulensi, bili za maji na oksijeni katika hospitali..

“Hii haikubaliki kwa sababu inamaanisha huduma zote za sekta yetu muhimu ya afya zitakwama,” Bi Waiguru aliwaambia madiwani.

Aidha, aliwalaumu madiwani hao kwa kuondoa Sh59 bilioni zilizotengewa idara ya sheria kulipa mawakili. Alisema uamuzi huo ungefanya serikali yake ishindwe kufuatilia kesi zaidi ya 200 nyingi zinazohusu ardhi iliyonyakuliwa.