Habari Mseto

Pigo kwa waundaji wa rangi yenye Lead

October 23rd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Watengenzaji wa rangi huenda wakapata pigo kubwa kutokana na hatua ya wahifadhi mazingira kusukuma kupigwa marufuku kwa matumizi ya madini ya Lead kutengeneza rangi.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) tayari limeyapa mataifa hadi 2020 kutekeleza agizo hilo.

Lead licha ya kuwa ni sumu hutumiwa kutengeneza rangi za kupaka nyumba kwa lengo la kuzipa rangi tofauti, kupunguza muda wa kukauka na kukinga dhidi ya maji.

Kulingana na WHO, inakadiriwa kuwa kuna visa 600,000 vipya vya watoto kukosa uwezo wa kuwa weledi miongoni mwa watoto kila mwaka.

“Kiwango chochote cha Lead sio salama,” ilisema WHO.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP) 2015 liliamua kuwa mataifa ya Afrika yalifaa kupunguza kiwango cha risasi hadi vipande 90 kwa milioni moja.

Hata hivyo, WHO sasa njia muafaka zaidi ya kukabiliana na sumu ya risasi ni kupitia udhibiti na marufuku.

Rangi nchini Kenya ina viwango vya juu sana vya Lead – 10,000 ppm.