Michezo

Pigo Northern Ireland baada ya mwanasoka tegemeo Corry Evans kupata jeraha la paja

November 8th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO Corry Evans atakosa mchuano wa mchujo wa kufuzu kwa fainali za Euro 2021 utakaokutanisha timu yake ya taifa ya Ireland ya Kaskazini na Slovakia mnamo Novemba 12, 2020.

Evans alipata jeraha baya la paja wakati wa mechi ya Ligi ya Daraja la Kwanza (Champioship) dhidi ya waajiri wake Blackburn Rovers na Queens Park Rangers (QPR) mnamo Novemba 7, 2020. Blackburn waliibuka washindi wa gozi hilo kwa mabao 3-1.

Kocha Tony Mowbray wa Blackburn amethibitisha kwamba Evans atafanyiwa tathmini ya kina na madaktari mnamo Novemba 9 kabla ya muda kamili atakaohitaji mkekani kuuguza jeraha kubainika.

Evans anajivunia kuvalia jezi za Ireland ya Kaskazini mara 64 tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza mnamo 2009.

Kujeruhiwa kwa Evans ni pigo kunwa kwa mkufunzi Ian Baraclough ambaye sasa atakosa sogora mwenye uzoefu mkubwa na tajriba pevu zaidi katika kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya kufa-kupona ya kufuzu kwa fainali za Euro 2021.

George Saville ambaye pia alikosa mechi iliyoshuhudia waajiri wake Middlesbrough wakiambulia sare tasa dhidi ya Brentford kwenye Championship mnamo Novemba 7 pia hatakuwa sehemu ya kikosi cha Ireland ya Kaskazini.

Evans aliyepata jeraha baya la kichwa mnamo Januari 2020 alipona upesi kinyume na ilivyotarajiwa na kurejea ugani mnamo Juni 2020. Ushirikiano mkubwa kati yake na nahodha Steven Davis ulidhihirika pakubwa kwenye mechi iliyowakutanisha na Bosnia-Herzegovina mnamo Oktoba 2020.

Ireland ya Kaskazini watakuwa wenyeji wa Slovakia ugani Windsor Park mnamo Novemba 12 katika mechi itakayohudhuriwa na mashabiki 1,000. Watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi katika mechi hiyo ili kufuzu kwa fainali za Euro kwa mara ya pili mfululizo.