Michezo

Pigo Real Madrid baada ya Hazard na Casemiro kuugua Covid-19

November 7th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

WANASOKA wawili wa Real Madrid – Eden Hazard, 29, na Casemiro, 28, wameugua Covid-19 na watalazimika sasa kujitenga kwa siku 14.

Hazard ambaye ni raia wa Ubelgiji na mwenzake ambaye ni wa timu ya taifa ya Brazik, sasa watakosa mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) itakayowakutanisha na Valencia ugenini mnamo Novemba 8, 2020.

Katika taarifa yao, Real wamesema kwamba visa hivyo viwili ndivyo vya pekee vilivyopatikana kambini mwao baada ya vipimo vya corona kufanywa ugani Alfredo Di Stefano mnamo Novemba 6, 2020.

Hazard na Casemiro wanauguza Covid-19 siku nne baada ya mwanasoka mwingine wa Real, Eder Militao, kupatikana na virusi vya homa hiyo hatari.

Hazard kwa sasa atakosa michuano ijayo ya kimataifa itakayopigwa na Ubelgiji mwezi huu wa Novemba, ikiwemo mechi ya UEFA Nations League dhidi ya Uingereza mnamo Novemba 15.

Mara ya mwisho kwa Hazard kuvalia jezi za Real ni katika mechi iliyowakutanisha na Inter Milan kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3, 2020. Real walishinda mechi hiyo 3-2 licha ya Hazard kupata jeraha la mguu katika kipindi cha pili.

Kwingineko, visa vingine viwili vya maambukizi ya corona vimeripotiwa na Shirikisho la Soka nchini Italia (FIGC). Mbali na kocha Roberto Mancini wa timu ya taifa ya Italia, mwanasoka Edin Dzeko wa klabu ya AS Roma pia ameugua Covid-19.

Mancini, 55, amewahi kudhibiti mikoba ya Manchester City kati ya 2009-13. Sasa atakosa mechi tatu zijazo ambazo zitakutanisha masogora wake na Estonia mnamo Novemba 11 kisha Poland na Bosnia kwenye UEFA Nations League.

Mancini aliwahi kuwatia makali wachezaji wa Inter Milan kwa misimu mitatu kabla ya kujiunga na Man-City aliowaongoza kutwaa ubingwa wa Kombe la FA mnamo 2011 na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2012.

Alipokezwa mikoba ya Italia baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi. Tangu wakati huo, ameongoza mabingwa hao wa Kombe la Dunia mnamo 2006 kusajili ushindi mara 10 kutokana na mechi 10 za kufuzu kwa fainali za Euro 2021.