Pigo Ruto akipoteza ‘jenerali’

Pigo Ruto akipoteza ‘jenerali’

Na WANDERI KAMAU

KAMBI ya kisiasa ya Naibu Rais, Dkt William Ruto iliendelea kuyumba Jumapili baada ya mbunge Didmus Barasa wa Kimilili kutangaza ‘kuchukua likizo ya muda’ ili kutathmini mwelekeo wake kisiasa.

Bw Barasa, ambaye ni miongoni mwa washirika wakuu wa Dkt Ruto kutoka eneo la Magharibi, alisema atachukua likizo ya miezi minne kutoka siasa ili kujaribu “kuunganisha” jamii ya Abaluhya.

Hatua hiyo inajiri wiki chache baada ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na mrengo wa ‘Tangatanga’ na Dkt Ruto kushindwa vibaya kwenye chaguzi ndogo katika maeneobunge ya Kabuchai na Matungu mapema mwezi huu.

Hilo pia linafuatia kushindwa vibaya kwa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo kwa useneta katika Kaunti ya Machakos, Alhamisi, ambapo Bi Agnes Kavindu wa chama cha Wiper aliibuka mshindi.

Bi Kavindu alizoa kura 104, 352 dhidi ya Bw Urbanus Ngengele wa UDA, aliyepata kura 19, 726 pekee.

Kwenye kikao na wanahabari nyumbani kwake katika eneo la Nasanda, eneobunge la Kimilili, Bw Barasa alitishia kujiondoa kwenye muungano huo ikiwa “hautatilia maanani maslahi ya jamii ya Abaluhya”.

“Ni lazima nihakikishe kuwa maslahi ya jamii ya Abaluhya yanazingatiwa ili kuendelea kuunga mkono mrengo huo. Nimejitolea kuwa muunganishi wa viongozi wote kutoka jamii hii ili kuhakikisha inafaidika kwenye uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Barasa.

Aliongeza, “Nitatumia muda huo kuwafikia viongozi kama Dkt Mukhisa Kituyi, mbunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, kwa lengo la kufanya kazi pamoja na kubuni chama kimoja cha jamii ya Mulembe.”

Hatua yake inajiri huku uvumi ukiendelea kuenea kuhusu uwepo wa malumbano na migawanyiko mikubwa katika kambi hiyo kufuatia matokeo hayo.

Washirika wa Dkt Ruto kama aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale, hawajaonekana hadharani kwa muda tangu chaguzi za maeneo ya Matungu na Kabuchai kutangazwa. Dkt Khalwale pia amekuwa miongoni mwa washirika wa Dkt Ruto katika eneo la Magharibi.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya siasa, huenda mwelekeo huo ukamwathiri sana Dkt Ruto kisiasa, ikizingatiwa amekuwa kwenye juhudi za kujenga mtandao wa washirika ambao watamsaidia kwenye kampeni zake za urais.

“Ni hali itakayopunguza sana umaarufu wa Dkt Ruto kitaifa. Kumekuwa na hali ya suitafahamu katika kambi hiyo (Tangatanga) baada ya matokeo ya chaguzi za Matungu na Kabuchai. Washirika zaidi wataendelea kuhama,” akasema mchanganuzi wa siasa Martin Andati, kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumapili.

Alisema kuna uwezekano mkubwa kwamba Dkt Khalwale vilevile anapanga kuhama kutoka mrengo huo.

“Boni (Khalwale) amekuwa akijaribu kumfikia Seneta Wetang’ula kichinichini. Hata Gavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) amekuwa akitafuta ushauri kutoka kwa wafuasi wake. Kuna uwezekano akahamia chama kingine cha kisiasa,” akasema Bw Andati.

Mchanganuzi wa siasa, Mark Bichachi alitoa kauli kama hiyo, akisema ni wakati Dkt Ruto anafaa kutathmini upya mwelekeo wake kisiasa, la sivyo huenda muungano wa ‘Tangatanga’ ukavurugika kabisa ifikapo mwaka 2022.

Licha ya hilo, baadhi ya waandani wa Dkt Ruto wanashikilia kuwa hali bado ni shwari kwenye kambi hiyo, wakitaja hayo kama matukio ya kawaida katika siasa.

You can share this post!

DIMBA: Jules Kounde ni kisiki kisichovuja ligini Uhispania

UDAKU: Kibibi Jocelyn Burgardt anavyomkimbiza Cavani polo...