Pigo West Ham beki tegemeo Kurt Zouma akiingia mkekani

Pigo West Ham beki tegemeo Kurt Zouma akiingia mkekani

Na MASHIRIKA

BEKI wa West Ham United, Kurt Zouma anatarajiwa kusalia mkekani kwa muda mrefu kuuguza jeraha la paja alilolipata wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowashuhudia wakipepeta Chelsea 3-2 mnamo Disemba 4, 2021.

Nyota huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 27 alifanyiwa tathmini ya madaktari mnamo Disemba 6, 2021 japo waajiri wake hawakufichua muda atakaohitaji kabla ya kurejea ugani. Beki mwenzake kambini mwa West Ham, Angelo Ogbonna anatarajiwa kukosa mechi zote zilizosalia kwenye kampeni za muhula huu kutokana na jeraha la goti alilolipata Novemba 2021.

Kutikisika kwa uthabiti wa safu ya nyuma ya West Ham ni jambo ambalo linatarajiwa kumchochea kocha David Moyes wa West Ham kujishughulisha sokoni mwanzoni mwa Januari 2022 kwa ajili ya kusajili difenda mpya.

Zouma amewajibishwa na West Ham katika kikosi cha kwanza ligini msimu huu mara 15 tangu aagane na Chelsea mwishoni mwa muhula wa 2020-21. Alikuwa nguzo muhimu katika safari ya kupanda kwa Chelsea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Huku Ogbonna akitazamiwa kusalia mkekani kwa muda, kocha Moyes sasa anasalia na madifenda Issa Diop na Craig Dawson pekee ikizingatiwa kwamba veterani Winston Reid aliagana na West Ham mnamo Septemba 2021.  Japo beki chipukizi Ben Johnson, 21, pia anauguza jeraha la misuli ya miguu, sogora huyo atarajiwa kurejea ulingoni mapema zaidi kuliko Zouma.

You can share this post!

Sharti uchaguzi uwe wa amani -Matiang’i

Kesi ya ufisadi ya Sh7.4Bn dhidi ya Mbunge Rigathi Gachagua...

T L