Michezo

Pipeline yaondolea Kenya aibu kipute cha voliboli Misri

March 26th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Pipeline kutoka Kenya imehifadhi medali ya shaba katika voliboli ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuchabanga GS Petroliers ya Algeria kwa seti 3-0 jijini Cairo nchini Misri, Jumatatu.

Vipusa wa Pipeline, ambao ndio timu ya pekee kutoka Kenya iliofika robo-fainali mwaka huu, walisherekea ushindi kwa densi na nyimbo kutwaa medali hiyo waliyovuna kwa kulemea Petroliers kwa alama 25-22, 25-17, 25-18 katika mechi ya kusisimua ya kutafuta nambari tatu.

Pipeline, ambao walipoteza wachezaji saba muhimu pamoja na kocha mkuu Japheth Munala kwa klabu ya KCB mwezi Desemba mwaka 2016, sasa wanajivunia medali 20 katika mashindano haya ya kila mwaka baada ya kutwaa dhahabu saba, fedha nane na shaba tano.

Mara ya mwisho walishinda kombe hili ni mwaka 2005 jijini Nairobi. Ushindi wao dhidi ya Petroliers hapo Machi 25 ni kisasi kitamu baada ya kupoteza katika fainali ya mwaka 2014.

Katika makala ya mwaka 2019, wawakilishi wengine wa Kenya, KCB, walimaliza katika nafasi ya tisa baada ya kulima Rwanda Revenue Authority (RRA) 3-0 Machi 24 nao mabingwa wa Kenya, Prisons, wamemaliza mkiani baada ya kujiondoa baada tu ya mechi za makundi.

Prisons ilikuwa na masaibu mengi mjini Misri ikiwemo kuamrishwa na Wizara ya Usalama wa Ndani kurejea nyumbani mara moja kwa kile wizara hiyo ilitaja “kuaibisha nchi” baada ya ripoti kwamba hoteli walimokuwa wakiishi ilitaka kuwafurusha kwa kutoilipa.

Fainali kati ya mabingwa mara tisa Al Ahly kutoka Misri na Carthage ya Tunisia ni leo Jumatatu.

Jedwali la mwaka 2019:

1.Al Ahly (Misri)/Carthage (Tunisia)

2.Carthage (Tunisia)/Al Ahly (Misri)

3.Pipeline (Kenya) 3-0 GS Petroliers (Algeria)

4.GS Petroliers (Algeria)0-3 Pipeline (Kenya)

5.El Shams (Misri) 3-0 Customs (Nigeria)

6.Customs (Nigeria) 0-3 El Shams (Misri)

7.FAP (Cameroon) 3-1 Sporting (Misri)

8.Sporting (Misri) 1-3 FAP (Cameroon)

9.KCB (Kenya) 3-0 Revenue Authority (Rwanda)

10.Revenue Authority (Rwanda) 0-3 KCB (Kenya)

11.Canon (Congo Brazzaville) 3-0 USFA (Burkina Faso)

12.USFA (Burkina Faso) 0-3 Canon (Congo Brazzaville)

13.Shooting (Misri) 3-0 DGSP (Congo Brazzaville)

14.DGSP (Congo Brazzaville) 0-3 Shooting (Misri)

15.Asec (Ivory Coast)

16.Nkumba (Uganda)

17.Prisons (Kenya)