Pixel Waite asema subira ni muhimu kwa kila msanii

Pixel Waite asema subira ni muhimu kwa kila msanii

Na JOHN KIMWERE

NI msanii wa kizazi kipya anayelenga makuu katika sekta ya muziki wa injili barani Afrika.

Dancan Ombima Ambuka maarufu Pixel Waite anasema anahisi anatosha anakolenga kuibuka kati ya wanamuziki mahiri nchini miaka ijayo.

Kando na muziki msanii huyu aliyezaliwa mwaka 1989 ni muigizaji, mchekeshaji, mratibu wa sherehe (MC) pia anamiliki kampuni iitwayo Waite Empire anayosimamia waigizaji pia wana mitindo.

”Ni kweli sijapata mashiko jinsi ninavyolenga ila ninaamini wakati utakapowadia hakuna atayezuia baraka zangu,” anasema na kuongeza kuwa la mno amezamia shughuli ya kuhubiri injili ya Mungu kupitia muziki.

Anafichua kwamba alianza kuvutiwa na utunzi akiwa shule ya msingi hasa alipogundua alikuwa gwiji wa kuandika mashairi. Anakariri kuwa uandishi wake wa mashairi ulimsaidia pakubwa katika uandikishi wa mistari ya nyimbo zake.

Tuzo

Ingawa alitunga na kurekodi nyimbo ya kwanza mwaka 2012 kibao cha ‘Waite waite’ alichoachia miaka mitatu baadaye ndicho kilichomtambulisha

katika ulingo wa muziki. Miaka mitano baadaye wimbo wake ‘Take over’ ulibahatika kufanya vizuri na kuchangia kuzoa tuzo kwenye hafla ya Fema Awards.

Daddy Owen

Msanii huyu anajiuvunia kughani zaidi ya fataki 100 ambapo amefanikiwa kurekodi vibao 50 huku 15 zikiwa kwenye mtandao wa kijamii wa youtube.

Ametunga nyimbo kama ‘Ananipenda,’ ‘Ni wewe,’ Wakati wangu,’ ‘Furaha ft Daddy Owen,’ ‘Waite waite,’ ‘Shangwe’ alioshirikisha Dr Ofweneke, ‘Power’, ‘Take Over’, na ‘Asante’ miongoni mwa nyingine.

Nyimbo zinazopatikana kwenye YouTube ni kama ‘Take over’, ‘One day’, ‘Asante’, ‘Ananipenda’, ‘Wakati’, ‘Njia zako’ na kibao ‘Furahia’ alichoshirikisha Daddy Owen kati ya vibao vingine.

Kwa sasa anatamba kwa kibao kiitwacho Nikuimbie, wimbo alioshirikiana na Joy Wanjiru na kuachia mwezi mmoja uliopita.

Dancan Ombima Ambuka maarufu Pixel Waite. PICHA | JOHN KIMWERE

Kama ilivyo kwa wanamuziki wengi anataja kuwa Afrika Mashariki anapenda kusikiliza tambo kama ‘Nyakati’ kazi yake mtunzi wa Bongo Goodluck Gozbert. Pia fataki yake Ekko Dydda iitwayo Reason bila kuweka katika kaburi la sahau fataki kwa jina Kazi ya Msalaba yake Daddy Owen.

Anadokeza kuwa mashabiki pia Wakristo wengi wamepoteza imani nao maana baadhi yao wanatumia muziki wa injili kama biashara.

”Suala hilo linatupatia wakati mgumu kwa kuzingatia limechangia wengi kusepa shoo za wanamuziki wa nyimbo za kumtukuza Mungu,” akasema.

Mawaidha

Anashauri wenzake wanaokuja akiwahakikishia kuwa subira inalipa wala wasiwe na pupa katika jukwaa la muziki wa injili.

”Kila msanii anapenda mafanikio kwa kazi zake ambapo hatuna budi kuamini ipo siku milango itafunguka,” akasema.

Wito

Anataka serikali itambue wasanii chipukizi pia kuweka mikakati ya kuwapa haki zao kupigania nafasi katika ulingo wa tasnia ya muziki.

Anadokeza kuwa kuna wasanii wengi nchini Kenya na kusisitiza wanaohitaji sapoti ili kutimiza maazimio yao.

  • Tags

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Suala la aliye mkarimu kati ya Raila na Ruto...

Makahaba wapigania pesa za Ruto

T L