Jamvi La Siasa

PK Salasya: Kwake kila hafla ni shajara ya vitimbi

January 13th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

ALIPOCHAGULIWA kama mbunge na wakazi wa eneobunge la Mumias Mashariki, hilo lilionekana kuwa mwanzo mpya wa kisiasa kwa Peter Salasya.

Ikizingatiwa kuwa alichaguliwa akiwa bado kijana, huo ulikuwa ushindi wa kipekee kwa Bw Salasya.

Kwa kawaida, huwa ni vigumu sana kwa vijana kushinda nyadhifa kubwa za kisiasa kama vile ubungehaoa nchini, kwani huwa kampeni zake zinahitaji fedha nyingi.

Hata hivyo, mbunge huyo ameibukia kuwa mbishi, kwa kuzua utata ndani na nje ya Bunge la Kifaifa.

Kinaya ni kuwa, licha ya kuandamwa na kila aina ya utata, amekuwa akiorodheshwa kuwa miongoni mwa wabunge wachapakazi zaidi nchini.

Mnamo Ijumaa, Bw Salasya alikamatwa kwa dai la kumshambulia diwani katika Kaunti ya Kakamega.

Hata hivyo, aliachiliwa baadaye kwa dhamana ya Sh50,000 akingoja kufikishwa mahakamani Jumanne.

Kwenye taarifa, polisi walisema kuwa kuna uwezekano atafunguliwa shtaka la kumshambulia mtu na kumjeruhi, jambo ambalo ni kinyume na Sehemu 251 ya Sheria za Kenya.

Kisa hicho kilifanyika wakati wa hafla ya mazishi katika eneo la Mumias, Ijumaa, Januari 12, 2023.

Mwaka uliopita, mbunge huyo alishtakiwa kwa kutishia kumuua hakimu aliyekuwa amemwagiza kulipa deni la Sh500,000 kwa mfanyabiashara mmoja. Ilidaiwa Bw Salasya alikuwa amekaa na deni hilo kwa miaka kadhaa, ndipo mfanyabiashara huyo akaamua kumfikisha mahakamani.

Hakimu Gladys Kiama wa Mahakama ya Mizozo Midogo Midogo ya Kakamega, alimwagiza Bw Salasya kumlipa mfanyabiashar Robert Lutta deni la Sh500,000 lililojumuisha riba na gharama ya kesi hiyo.

Mfanyabiashara huyo alifika mahakamani akimtaka mwanasiasa huyo kumlipa fedha hizo, baada ya kumkopea mnamo Desemba 13, 2022. Walikuwa wamekubaliana kuwa Bw Salasya angemlipa baada ya miezi miwili.

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ilimkashifu mbunge huyo kwa kutoa vitisho hivyo, huku ikianza uchunguzi kuhusu suala hilo.

Mnamo Novemba mwaka uliopita, Bw Salasya alishambuliwa na kufukuzwa kutoka ibada katika Kanisa la Katoliki la Bukaya, eneobunge la Mumias Magharibi na vijana wenye hasira.

Bw Salasya alikuwa akitoa hotuba yake wakati mtu mwenye hasira alimnyang’anya kipaaza sauti.

Kisa hicho kilifanyika wiki mbili tu, baada ya wakili katika Kaunti ya Kakamega kumshtaki Bw Salasya kwa dai la kumshambulia.

Inadaiwa Bw Salasya alimshambulia Wakili Edwin Wawire kwa kundesha kesi iliyomkabili kwa kutolipa deni la Sh500,000.

Suala hilo bado liko mahakamani.

Bw Salasya pia amezua utata kwa kutangaza sifa za mwanamke ambaye angetaka awe mkewe.

Alisema kuwa  lazima awe kati ya miaka 23 na 26, ila alitoa ilani: mwanamke huyo hatakuwa akiangalia simu yake!

Mnamo Februari 2023, alizua utata mwingine alipotoa matamshi ya udhalilishaji wa kijinsia kumhusu Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Bomet, Linet Chepkorir ‘Toto’,  kwa madai ya kutomheshimu kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga.

Hata hivyo, alilazimika kumwomba msamaha mbunge huyo.

Soma Pia: PK Salasya alia baada ya ‘kulemewa’ na bei ya viatu nchini Afrika Kusini