Bambika

PK Salasya na DJ Pierra Makena wamezeana mate ‘kufanya biashara’

February 22nd, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya na DJ Pierra Makena wanamezeana mate kiujanja, kila mmoja akitafuta fursa ya kukutana na mwenzake kunong’onezana mawili matatu.

Hii ni baada ya mcheza santuri, Pierra, katika mahojiano yake na Oga Obinna kufichua kuwa anammezea mate mbunge huyo.

Wakati wa  shoo ya Comedy and Vibe iliyoandaliwa na MC Tricky, Bw Salasya alisema aliwahi kukutana na Pierra mara moja na yuko tayari kukutana naye kwa mara nyingine.

“Watu wanaponipenda huwa najisikia vizuri sana. Mwambie tu mimi pia namtafuta na aendelee kunitafuta. Nimemuona kwa mara ya kwanza lakini mtaniambia siku anakuwa na shoo ili nihudhurie nijue kwa jinsi gani anavyopanga kazi yake. Anacheza reggae ama anacheza ngoma gani vile?” akauliza Bw Salasya.

Tracy Kush alimfahamisha mbunge huyo kuwa mcheza santuri huyo amebobea katika aina zote za muziki.

Jibu hilo lilimpa Bw Salasya wazo la kutaka wanaomhoji kufahamu kuwa atamtafuta kushirikiana kibiashara.

“Mwambie tu nitakuja kwa gig yake,” akasema Bw Salasya.

Mbunge huyo aliongeza kuwa suala la mahusiano hutegemea jinsi mambo yanavyoenda baada ya wawili wa jinsi tofauti kufahamikiana.

“Tutaona jinsi mambo yatakavyoenda. Mambo ni polepole,” akaweka wazi.

Wiki moja imepita baada ya mcheza santuri huyo mwenye umri wa miaka 42 kukiri ‘kumfagilia’ sana mbunge huyo.

Katika mahojiano na Oga Obinna, alifichua sababu ya kutoolewa, akisema kakosa mume sahihi.