Pochettino aanza kazi ya ukocha PSG kwa sare dhidi ya St-Etienne ligini

Pochettino aanza kazi ya ukocha PSG kwa sare dhidi ya St-Etienne ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino alishuhudia mechi yake ya kwanza kusimamia kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) ikikamilika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Saint-Etienne.

Matokeo hayo yaliwezesha Olympique Lyon ambao kwa sasa wamejizolea pointi 39 kufungua mwanya wa alama tatu kati yao na PSG kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya kuwapokeza Lens kichapo cha 3-2.

Alama 36 ambazo PSG wameokota kutokana na mechi 18 zilizopita zinawiana na idadi ya pointi zinazojivuniwa na nambari tatu Lille.

Romain Hamouma alichuma nafuu kutokana na masihara ya kiungo Idrissa Gueye katika dakika ya 19 kabla ya Moise Kean wa PSG kusawazisha mambo dakika tatu baadaye.

Chini ya Pochettino aliyeaminiwa kuwa mrithi wa kocha Thomas Tuchel aliyetimuliwa mnamo Disemba 24, PSG waliwaruka Lille jedwalini kwa wingi wa mabao baada ya Lille kuduwazwa na Angers waliowapokeza kichapo cha 2-1.

Licha ya kutamalaki mechi na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, PSG walishindwa kufanya mashambulizi makali langoni mwa Saint-Etienne waliopania kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa kwenye jumla ya mechi saba mfululizo.

Mbali na Hamouma, wachezaji wengine waliomweka kipa Keylor Navas wa PSG katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada mwishoni mwa kipindi cha pili ni Mathieu Debuchy na Denis Bouanga.

Nusura Angel di Maria na Pablo Sarabia wafungie PSG mabao mawili ya haraka dakika chache kabla ya mchuano kukamilika ila kipa Jessy Moulin akajitahidi maradufu kupangua makombora yao.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Januari 6):

St-Etienne 1-1 PSG

Brest 2-0 Nice

Lorient 2-5 Monaco

Metz 0-0 Bordeaux

Nantes 0-0 Rennes

Strasbourg 5-0 Nimes

Lille 1-2 Angers

Lyon 3-2 Lens

Marseille 3-1 Montpellier

Reims 0-0 Dijon

You can share this post!

Kang’ata acheza kama yeye

Man-City kuvaana na Spurs kwenye fainali ya Carabao Cup...