Michezo

Pochettino aomba radhi baada ya farakano baina ya wachezaji wa Spurs na Manchester United

July 27th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKI

KOCHA wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino ameomba msamaha Manchester United baada ya wachezaji wake kuvyoga mahasimu hao katika mechi ya kujipima nguvu siku ya Alhamisi.

Katika joto kali mjini Shanghai, kiungo Moussa Sissoko aliponea kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumkung’uta kwa miguu Daniel James, tukio lililozua fujo kutoka kwa wachezaji wa klabu zote mbili.

Dele Alli pia alilishwa kadi ya njano kwa kukanyaga Man United mara mbili, huku Andreas Pereira wa United pia akikula kadi sawa na hiyo.

Baada ya mechi, ambayo Spurs ilipoteza 2-1, Pochettino alisema, “Naomba msamaha Manchester United kwa niaba ya wachezaji wetu.

“Nilikerwa kidogo na matukio kadhaa. Sikufurahishwa kwa sababu wakati mwingine unaweza kukabili mchezaji ukiwa umechelewa halafu kitu kitendeke.

“Wakati mwingine unahitaji kuonyesha nguvu zako na kucheza kwa ari, lakini umuhimu ulikuwa kujiweka katika hali nzuri na kuimarisha mchezo wetu.”

Hata hivyo, kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer hakuonekana kuhuzunishwa na mchezo ambao wachezaji wake walikumbana nao.

Solskjaer alisema, “Sina hofu. Soka ni mchezo wa kushindana na tunajiandaa kwa ligi. Sikuona soka ambayo mtu alitembea kwa kutumia vidole.

“Hatukupondwa kwa miguu. Tulijibu vilivyo. Kivyangu, naona ulikuwa mchezo mzuri sana.”

Mshambuliaji chipukizi Angel Gomes, 18, alifungia United bao la ushindi zikisalia dakika 10 mechi itamatike. Lucas Moura alikuwa amesawazishia Spurs 1-1 dakika ya 65 baada ya Anthony Martial kufungua ukurasa wa magoli dakika ya 21.

Gomes alishirikiana vyema na Juan Mata kabla ya kumwaga kipa Paolo Gazzaniga na kuendeleza rekodi ya United kutoshindwa hadi mechi nne.

Bailly aumia

Hata hivyo, mambo hayakuwa tu mazuri kwa United kwa sababu beki Eric Bailly aliondoka uwanjani Hongkou akitembea kwa mikongojo baada ya kuumia goti katika kipindi cha pili.

Bailly alionekana kuteleza, bila ya kuguswa, huku akijaribu kufuata na kuzuia mshambuliaji matata Heung-min Son kuingia ndani ya kisanduku. Bailly kisha aliondolewa uwanjani kwa kubebwa kwa machela.

Solskjaer aliongeza, “Si vizuri kabisa unapopata jeraha.” “Hatuna uhakika ubaya wa jeraha hilo. Eric atafanyiwa uchunguzi mjini Manchester na tunatumai atakuwa sawa.”

Wakati huo huo, kwa mara ya pili chini ya wiki mbili, Darcie Glazer Kassewitz, mmoja wa watoto sita wa Glazer ambaye anamiliki United, amechukua mkopo kutoka benki moja nchini Marekani akitumia hisa zake za Manchester United kama dhamana.

Mapatano hayo, ambayo yaliafikiwa Julai 23 lakini ndipo yametangazwa rasmi, yanaonyesha Glazer Kassewitz alitoa dhamana ya hisa 773,000 ya kiwango chake cha Kundi B cha hisa za kawaida, ambazo thamani yake ni Sh1.4 bilioni.

Glazer Kassewitz bado atasalia na haki zake za kupiga kura na pia haki za kupokea faida zinazotokana na kumiliki hisa hizo, “isipokuwa akikosa kulipa mkopo huo jinsi walivyokubaliana.”