Habari Mseto

Poda 'hatari' ya Johnson & Johnson yachunguzwa

February 23rd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

PODA ya wototo inayotengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson inachunguzwa kuhusiana na hofu kwamba ina chembechembe hatari za asbesto.

Poda ya Johnson &Johnson hutumiwa na wazazi wengi kupaka watoto wao wachanga, na pia hutumiwa kwa namna tofauti.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilisema kuwa inashirikiana na mashirika ya uchunguzi katika uchunguzi huo.

Kampuni hiyo ilipelekwa mahakamani na wateja wake kufikia 13,000 waliodai kuwa poda yake ina asbesto, ambayo huaminika kusababisha kansa tofauti.

Mwaka 2018, ripoti ilichapishwa na baadhi ya magazeti kama vile New York Times na Reuters kuhusiana na mawasiliano ya ndani katika kampuni kuhusiana na athari za asbesto katika bidhaa zake za poda.

Madai hao yalifanya kampuni hiyo kupata hasara kubwa katika soko la hisa ambapo hisa zake zilishuka kwa zaidi ya asilimia 12.

Licha ya habari hizo, kampuni hiyo imezidi kujitetea kuhusiana na usalama wa bidhaa zake kwa kusema poda yake haisababishi kansa kulingana na uchunguzi uliofanywa na mahabara kubwa.